• Nairobi
  • Last Updated April 17th, 2024 6:55 PM
Wanakandarasi Murang’a walia kudaiwa hongo na wanasiasa

Wanakandarasi Murang’a walia kudaiwa hongo na wanasiasa

NA MWANGI MUIRURI
 
WANAKANDARASI katika Kaunti ya Murang’a wamedai kwamba baadhi ya wanasiasa wa mrengo wa serikali huitisha hongo ili wawaidhinishie kandarasi.
Wamesema baadhi wa wabunge na madiwani ndio wanasumbua ajabu hasa katika ujenzi wa barabara.

“Baadhi ya kandarasi hizi ni lazima ziidhinishwe na kamati za wanasiasa hawa. Wanadai hongo ya kati ya asilimia 20 na 30 ya ujumla wa kandarasi. Hiyo ndiyo faida yetu. Wanataka tufanye kazi ya bure wao wakivuna faida,” yasema barua ya tetesi kutoka kwa muungano wa wanakandarasi eneo la Kati.

Barua hiyo ya Agosti 8, 2023, inasema kwamba hali ni mbaya kiasi kwamba baadhi ya kandarasi zimekwama kwa kuwa haiwezekani hongo hizo kutolewa.

“Tunampongeza Mbunge wa Kiharu Ndindi Nyoro kwa kuwa kwake hakuna shida hii ya ukandamizaji. Lakini katika baadhi ya maeneobunge mengine (majina yametajwa lakini tunayabana), ufisadi umekolea na Rais William Ruto anafaa ajue,” barua hiyo yasema.

Barabara ambazo zimetajwa kulengwa zaidi na hali hii ni zile zinazojengwa kwa kutumia hazina ya mamlaka ya barabara za mashinani (Kerra).

Wanakandarasi hao wameteta kwamba hata wakipeleka tetesi zao kwa wahandisi wasimamizi wa eneo hilo, “wanatuambia kwamba hawana uwezo wa kudhibiti kamati za wanasiasa za kuidhinisha utekelezaji wa kandarasi”.

Wanakandarasi hao wameteta kwamba maovu ambayo yanatekelezwa na wanasiasa katika safu ya kandarasi ni mengi kiasi kwamba wenyeji wataumia na pia serikali ya Rais Ruto ipigwe vita kwa kuonekana kutojali.

“Hawa wanasiasa wengine wanazindua barabara zilizofadhiliwa na hata wahisani wa kimataifa lakini wanatoa taarifa za kusema zimefadhiliwa na pesa za umma. Uongo wa kuiba pesa ndio huo,” wasema.

Wanakandarasi hao pia wameteta kwamba baadhi ya wanasiasa hao wamekataa kuidhinisha malipo yao kabla ya kupewa hongo.

“Safari hii ni kama baadhi ya wapigakura wamechagua fisi wengi walafi kuwa viongozi. Wengi wao wana tamaa isiyoeleweka na tusipochunga, tutaharibu sera ya serikali ya Bottom-Up,” barua hiyo yasema.

[email protected]

  • Tags

You can share this post!

Ruto hoi kutetea urais huku viongozi Mlima Kenya wakipasha...

AMINI USIAMINI: Antpitta ni ndege mwenye soni akimwangalia...

T L