• Nairobi
  • Last Updated April 16th, 2024 6:55 PM
Wanawake wavamia nyumba na kunyakua mume wa wenyewe

Wanawake wavamia nyumba na kunyakua mume wa wenyewe

NA STEPHEN ODUOR

MWANAMKE mjini Garsen, Kaunti ya Tana River, alipigwa na butwaa baada ya wanawake wawili ambao amekuwa akiwakashifu kwa madai ya kumtongoza mumewe, kuvamia nyumba yake usiku na kumchukua mumewe.

Imedaiwa kuwa mwanamke huyo, Bi Asha, amekuwa akituma jumbe za vitisho na matusi kwa Bi Janet Mwende na Bi Celestine Makena, akiwataka kukoma mahusiano na mume wake.

Baadhi ya jumbe za simu ambazo wanawake hao walifichua zilionyesha amekuwa akiwaita makahaba na kuwatishia kuwaroga kwa kumnyemelea mumewe.

Kulingana na Bi Makena, ambaye anafanya kazi katika baa mjini humo, mume huyo alikuwa rafiki tu wa kawaida na mteja katika baa hiyo.

Makena alisema ashamwambia mara nyingi Bi Asha kwamba hakuna uhusiano wowote wa kimapenzi kati yao lakini bado huwa hamwamini.

“Sijawahi kuwa na uhusiano wa kimapenzi na mwanamume huyo. Tulikuwa marafiki lakini mengi tuliyokuwa tukifanya pamoja awali yalikoma alipooa. Nilimweleza huyo mwanamke haya lakini hasikii, anaendelea kunitukana tu,” akasema.

Kwa upande wake, Bi Mwende alisema aliingia hofu kwa sababu ya jumbe alizokuwa akitumiwa kwa simu na ikabidi asafiri bara na kuzima simu yake ili kupata amani.

Lakini aliporudi mjini, anadai kuwa mwanamke huyo alimwandama tena kwa jumbe na simu.

“Nilirudi tayari kukabiliana naye. Nilijua anabweka tu na nikamuonya kuwa asipoacha nitamchukua huyo mwanaume kwa sababu naye pia amechoka na fujo za mke wake,” akasema Bi Mwende.

Jumamosi jioni, Mei 27, 2023 wanawake hao wawili walivamia nyumba hiyo baada ya mwanamke huyo kumtumia Bi Makena ujumbe wa kumtahadharisha ajiepushe na mumewe.

Wakati huo, mume huyo ambaye ni afisa wa polisi, alikuwa amewasili Garsen kutoka Lamu.

Wawili hao pamoja na wanawake wengine ambao wamekumbwa na matusi kutoka kwa mwanamke huyo walienda na kumtoa mwanamume huyo kutoka nyumbani hadi kwa baa mjini Garsen na kumwacha Bi Salim kwa mshangao.

Walioshuhudia kisa hicho walisema, mwanamume huyo alionekana kufurahia mvutano wa wanawake na mkewe, kisha akakaa kilabuni hadi asubuhi aliporudi nyumbani.

Majirani wanafichua aliporudi, alikutana na mkewe mlangoni akiburuta mikoba yake nje ya nyumba.

“Alimuuliza tu alikokuwa akienda ila hakujibu. Jamaa alicheka tu, akaingia ndani ya nyumba akimuacha mkewe ajipange,” akasema Bi Janice Njeri, jirani.

Hata hivyo, mke huyo hakusafiri kama alivyokusudia na alionekana baadaye jioni akirudi ndani ya nyumba yake.

Katika mojawapo ya jumbe zilizofichuliwa, ilidaiwa alimwambia Bi Makena kuwa, “Mtajua mimi ni mtoto wa Kidigo, sishiriki chombo na mtu, nitawatia adabu, mkizidi nitawatumia majipu mteseke mpaka mimi.”

 

  • Tags

You can share this post!

Raha tele Vihiga wakinyanyua ubingwa wa Ligi Kuu

Ezekiel Mutua: Mchungaji wako si babako au mamako, komeni...

T L