• Nairobi
  • Last Updated April 17th, 2024 6:55 PM
Washukiwa kusalia seli siku 10

Washukiwa kusalia seli siku 10

WYCLIFFE NYABERI na CHARLES WASONGA

WANAUME wanne wanaoshukiwa kuwateketeza wanawake wakongwe kwa tuhuma za uchawi eneo la Marani, Kaunti ya Kisii, watasalia rumande kwa siku 10 zaidi uchunguzi unapoendelea.

Wanne hao; Amos Nyakundi Ondieki, Chrispine Ogeto Mokua, Peter Angwenyi Kwang’a na Ronald Ombati Onyonka walifikishwa katika mahakama moja mjini Kisii, jana Jumanne kufunguliwa mashtaka kuhusiana na mauaji hayo.

Walifikishwa mbele ya Hakimu Mkuu Mwandamizi wa Mahakama hiyo Paul Mutai katika mahakama hiyo japo hawakuruhusiwa kujibu mashtaka.

“Baada ya kusikiliza pande zote kwa makini, natoa agizo washukiwa wasalie rumande kwa siku kumi ili kuruhusu upande wa mashtaka kumaliza uchunguzi wao,” akasema.

Washukiwa wanadaiwa kushirikiana na watu wengine ambao hawakuwa mahakamani, kuwashambulia wanawake hao wenye umri wa miaka 60 kwenda juu.

Kisa hicho kilitokea usiku wa kuamkia Jumapili.

Ombi la wakili wa washukiwa hao Shaffin Kaba kutaka waachiliwe kwa dhamana lilikataliwa na Hakimu Mutai aliyeamuru wazuiliwe korokoroni.

Bw Kaba alieleza mahakama kuwa washukiwa hao ni watu wenye familia na kuwekwa kwao kizuizini kutawakosesha nafasi ya kuchuma mapato ya kujisaidia.

“Naomba wateja wangu waachiliwe kwa dhamana kwa sababu wao ndio tegemeo kwa familia zao. Na hawawezi kukataa kufikia mahakamani. Kuzuiliwa kwao kuchangia wake na watoto wao,” akaongeza.

Hata hivyo, Bw Mutai alikataa ombi hilo na kuamuru kuwa kesi itajwe mnamo Oktoba 29, 2021 wakati ambapo atatoa mwelekeo zao.

Wakati huo huo, Mbunge wa Kitutu Chache Kaskazini Jimmy Angwenyi jana Jumanne alilaani tukio hilo la Jumapili na kuwashauri wakazi kukoma kuchukua sheria mikononi mwa kwa kuwateketeza washukiwa wa uchawi.

“Ikiwa mtu fulani anashukiwa kuwa mchawi kile wananchi wanafaa kufanya ni kupiga ripoti kwa polisi. Wananchi hawana haki au idhini ya kuwashambulia na kuwaua washukiwa,” Bw Angwenyi akasema kwenye kikao na wanahabari katika majengo ya bunge, Nairobi.

Mbunge huyo aliwataka wakazi wa eneo hilo kukumbutia mafunzo ya kidini na kukoma kuendeleza ushirikina.

Kiongozi huyo aliwataka maafisa wa polisi kuwasaka washukiwa zaidi walioshiriki katika mauaji ya akina mama hao katika eneo la Marani.

“Nafurahi kuwa washukiwa wanne wamekamatwa. Lakini wengine walioshirikiano nao na ambao bado wanajificha wanafaa kukamatwa na kuwasilishwa mahakamani,” Bw Angwenyi akaongeza.

You can share this post!

Waiguru amtaka rais azungumzie mrithi wake

Man-City wang’aria Club Brugge huku chipukizi Cole...

T L