• Nairobi
  • Last Updated April 16th, 2024 7:55 AM
Washukiwa wa uvamizi wa shamba la familia ya Kenyatta kufikishwa mahakamani

Washukiwa wa uvamizi wa shamba la familia ya Kenyatta kufikishwa mahakamani

NA CHARLES WASONGA

WAZIRI wa Usalama wa Ndani Profesa Kithure Kindiki mnamo Jumatano, Mei 31, 2023 ametangaza kuwa washukiwa kadha watafikishwa mahakamani kuhusiana na uvamizi uliofanyika katika shamba la familia ya Rais mstaafu Uhuru Kenyatta mapema mwaka huu katika eneo la Ruiru, Kaunti ya Kiambu.

Kwenye kikao na wanahabari nje ya afisi yake iliyoko Jumba la Harambee, Profesa Kindiki amesema uchunguzi kuhusu kisa hicho umekuwa ukiendelea na “hivi karibuni washukiwa watawasilishwa kortini.”

Waziri alisema uchunguzi kuhusu uvamizi huo umechukua muda mrefu kwa sababu tukio hilo liliingizwa siasa.

“Kile kilichotendeka katika shamba la Northlands ni uhalifu mbaya zaidi. Kweli tumekuwa tukiendesha uchunguzi na hivi karibuni washukiwa watawasilishwa kortini kujibu mashtaka,” akasema Profesa Kindiki.

Akaongeza: “Uchunguzi huo umechukua muda mrefu kwa sababu ya kuingizwa siasa katika jambo hilo. Lakini awali nimewaambia Wakenya kuwa serikali hii haitaki kuingiza siasa katika masuala ya usalama wa kitaifa.”

Profesa Kindiki alikariri kuwa washukiwa wote wa uhalifu nchini watachukuliwa hatua za kisheria bila kujali miegemeo yao ya kisiasa.

“Hata baadhi ya viongozi wanaoegemea mrengo wa serikali watachukuliwa hatua za kisheria. Miongoni mwao ni wale ambao wamekuwa wakichochea uvamizi wa mashamba ya majani chai katika kaunti za Kericho na Bomet. Wanasiasa kama hawa wa Kenya Kwanza watakamatwa baada ya uchunguzi kukamilika,” akasema Profesa Kindiki.

Karibu kondoo 1, 500 waliibwa katika shamba la Northlands baada ya genge la wahuni walioonekana kukodiwa kuvamia shamba la Northlands.

Watu hao ambao walikuwa wamejihami kwa mapanga na mashoka walikata ua la shamba hilo na kuanza kuharibu mali kwa kukata miti na kuteketeza sehemu ya shamba hilo.

Uvamizi katika shamba hilo la famila ya Bw Kenyatta ulifanyika siku moja na uvamizi katika kampuni ya gesi ya kiongozi wa Azimio Raila Odinga, hali iliyochangia kuibuka kwa uvumi kwamba mashambulio hayo yalipangwa kulipiza kisasa dhidi ya viongozi wa upinzani.

  • Tags

You can share this post!

Azimio wazima mazungumzo ya maridhiano hadi wakati...

Shakahola: Awamu ya pili ya upasuaji maiti yakamilika...

T L