• Nairobi
  • Last Updated February 29th, 2024 5:56 PM
Watanzania mitandaoni wawafafanulia Wakenya maana ya neno ‘bibi’

Watanzania mitandaoni wawafafanulia Wakenya maana ya neno ‘bibi’

Na MARY WANGARI

 

WAKENYA Jumatatu wameungana na jamii ya kimataifa kumboleza kifo cha Mama Sara Obama kwa kutuma risala zao za rambirambi kwenye mitandao ya kijamii ya Facebook na Twitter.

Hata hivyo, ujumbe mojawapo kutoka kwa mwanahabari wa Tanzania Millard Ayo, ulionekana kuwakanganya Wakenya baada ya kutumia neno ‘bibi’ambalo ni neno la Kiswahili sanifu linalomaanisha ‘nyanya.’

“Sarah Obama ambaye ni Bibi wa Rais Mstaafu wa Marekani Barack Obama, amefariki dunia katika Hospitali ya Jaramogi Oginga Odinga Kisumu nchini Kenya akiwa na umri wa miaka 99, familia imethibitisha,” alisema Ayo.

Wakenya hutumia jina ‘bibi’ aghalabu kumaanisha ‘mke’ na ‘nyanya’ au ‘shosho’ (linalotokana na lugha ya Kikuyu) kumaanisha mamake mama, hivyo wengi walihisi ujumbe huo ulikuwa na walakini.

Katika juhudi za kuwafahamisha wenzao wasioelewa kuhusu maana ya neno hilo, wanamitandao kutoka Tanzania walijitokeza kwa jumbe za kuvunja mbavu huku wakirekebisha Wakenya kuhusu lugha ya Kiswahili.

“Sisi huku Kenya-Kakuma hatuna hicho kitu kinaitwa ‘bibi’ sisi tunasema ‘nyanya’  au ‘shosho’, hiyo ‘bibi ‘ni ya huko kwenu TZ,” Choto Mtaki alisema.

“Ati bibi? Ni nyanya ya Rais Obama sio bibi……ni shosho,” Wakenya wengine kwa kutojua walidhihirisha kutofahamu kwao.

“Bibi au Nyanya? Watanzania mbona mnafidhulika Kiswahili? Kama nyinyi ndio mnaparagaza Kiswahili hivi sembuse wanyonge wa lugha toka Uganda?” alifoka Adede Owalla

“Sisi uku Kenya labda ‘bibi’ tunayoijua tu ni BBI lakini kwetu ni shosho/nyanya,” Luhya Boy alidakia.

“Ukisema Bibi kwa wakenya ni mke, sema Nyanya au Shosh, pole Obama na familia  yote,” Teddy Bukwimba akasema.

 

“Watu wakisoma Kiswahili wewe ulikuwa unacheza na kokoto kwa locker! Chukua Kiswahili Kitukuzwe kwa bill yangu,”College Jokes alitoa dhihaka.

“Mwenzetu hapa alisahau karo yake shuleni manake hakuhitimisha matumizi yake ya karo wakati wa somo la Kiswahili. ‘Bibi’ ina maana ya nyanya basi,” Mtanzania Lubumbashi Kinshasa akawakosoa Wakenya.

“Bibi ni neno sahihi la Kiswahili linalomaanisha nyanya. Nitakutumia bili ya kukufunza hayo,” akaeleza Haron Ototo.

You can share this post!

Gavana Nyong’o aongoza Nyanza kumuomboleza Mama Sarah...

Mama Sarah Obama kuzikwa Jumanne