• Nairobi
  • Last Updated February 25th, 2024 10:30 AM
Watu sita waaga dunia Kikopey baada ya lori kupoteza mwelekeo na kuwagonga

Watu sita waaga dunia Kikopey baada ya lori kupoteza mwelekeo na kuwagonga

NA MWANGI MUIRURI

WATU sita wameripotiwa kuaga dunia katika mtaa wa Kikopey, Kaunti ya Nakuru huku wengine wakiachwa na majeraha mabaya baada ya lori kupoteza mwelekeo Jumapili usiku na kugonga wapitanjia kabla ya kubonda jengo moja.

Wakati wa ajali, waliokuwa wameangamia walikuwa watano lakini mtu mmoja zaidi ameaga dunia asubuhi katika hospitali ya Gilgil na kufikisha idadi kuwa sita.

Kwa mujibu wa kamanda wa polisi wa Gilgil Bw Francis Tumbo, kando na wapitanjia wawili waliouawa na lori hilo, wengine walikuwa ndani ya jengo moja la mabati wakicheza mchezo wa ‘pool table’.

Kati ya wachezaji hao ambao walikuwa 12 na ambapo watatu walipoteza maisha huku sita wakipata majeraha nao wanne wakifanikiwa kutoroka mauti hayo yaliyowatembelea usiku.

“Waliojeruhiwa walikimbizwa katika hospitali ya Gilgil huku walioaga dunia wakipelekwa katika hifadhi ya wafu ya eneo hilo la Gilgil,” akasema.

Bw Tumbo alisema kwamba ajali hiyo ya mwendo wa saa nne usiku iliacha magari mengine matatu yakiwa yameharibika vibaya baada ya kugongwa na lori hilo.

“Aidha, jengo hilo walimokuwa wachezaji wa ‘pool table’ liliharibika vibaya. Walioangamia wote walikuwa ni wanaume. Tunaendelea kumsaka dereva wa lori hilo ambaye alihepa baada ya ajali hiyo,” akasema.

Afisa huyo wa polisi alizidisha tahadhari kwa watumizi wote wa barabara akiwataka wamakinikie usalama wao kupitia kuchukua tahadhari.

“Ajali husemwa kwamba haina kinga lakini katika hali nyingine, utundu wetu ndio hutuponza. Kuna zile ajali ambazo tunaweza tukaepukana nazo kupitia tu kuwa waangalifu. Hasa katika msimu huu wa Krismasi na kuelekea sherehe za Mwaka Mpya, tunafaa tuwe waangalifu zaidi ili tujiepushie kilio cha mauti barabarani,” akasema.

[email protected]

  • Tags

You can share this post!

Mashirika yapigania haki ya ‘boychild’ visa vya...

Sasa madiwani watishia kumbandua Naibu Gavana wa Trans Nzoia

T L