• Nairobi
  • Last Updated March 5th, 2024 5:55 AM
Wauzaji bangi wanavyotumia magari ya kifahari kuisafirisha

Wauzaji bangi wanavyotumia magari ya kifahari kuisafirisha

NA FARHIYA HUSSEIN

OPERESHENI zinazoongozwa na Idara ya Upelelezi wa Makosa ya Jinai (DCI) zimegundua matumizi ya magari ya kifahari katika kusafirisha dawa za kulevya.

Idara ya upelelezi imeona uwiano ambapo idadi kubwa ya magari yanayohusika katika shughuli hizi zisizo halali kuwa ya kifahari.

Iwe ni gari aina ya sedan au SUV magari haya yanaonekana kutumika mara kwa mara katika usafirishaji wa dawa za kulevya.

Kisa cha hivi majuzi kilihusisha gari aina ya Toyota Harrier, lililonaswa wakati wa uchukuzi wa dawa za kulevya siku ya Jumatano, ambapo watu wawili walinaswa wakiwa na kilo 477 za bangi, yenye thamani ya takriban Sh14 milioni, kwenye barabara kuu ya Mombasa-Malindi.

Wawili hao, George Nitti (37) na Raphael Mbithi (37) walikamatwa katika eneo la Swallows, Kilifi Kusini operesheni iliyotekelezwa na Maafisa wa Polisi wanaohudumu chini ya DCI.

Operesheni hiyo ilisababisha kutwaliwa kwa gari aina ya Toyota Harrier, lililosajiliwa nambari KDK 020 B, lililokuwa likitumika kusafirisha dawa hizo haramu.

Kulingana na ripoti ya polisi iliyowasilishwa katika Kituo cha Polisi cha Ndonya katika eneo bunge la Kilifi Kusini, dereva aligoma kusimamishwa, na kuwalazimu maafisa kufyatua risasi kwenye tairi la kulia.

Dawa zilizonaswa, zilizochunguzwa na mwanakemia wa serikali Mombasa, zilifikisha kilo 477 zikiwa na thamani ya soko inayokadiriwa kufikia Sh14 milioni.

Hii sio mara ya kwanza kwa magari ya kifahari kuonekana yakitumika kusafirisha dawa za kulevya.

Septemba 4, 2023, operesheni nyingine ya DCI ilisababisha kunaswa kwa gari leusi aina ya Prado TX lililokuwa likitumiwa kusafirisha dawa za kulevya.

Katika tukio hilo, bangi kilo 316, yenye thamani ya Sh9 milioni, ilipatikana baada ya gari hilo kupata ajali na kutua kwenye mtaro.

Wakati wa uchunguzi, wapelelezi waliweza kupata nambari nyingi za usajili, KBQ 580K, KBZ 528N, KDA 639A, na KDC 947C zinazofanana na zile zinazoonekana kwenye magari ya umma, jambo ambalo lilizua shaka zaidi.

Huku barabara kuu ya Mombasa-Malindi ikionekana kuwa sugu katika usafirishaji wa dawa hizo haramu, mamlaka imeweka wazi msimamo wao kuhusu vita dhidi ya utumizi wa dawa za kulevya katika eneo la pwani na nchini kwa jumla.

Mwaka jana, Rais William Ruto alitangaza vita dhidi ya walanguzi wa dawa za kulevya na wauzaji mihadarati, akihakikishia umma kwamba utawala wake utakabiliana na tatizo la dawa za kulevya katika eneo la pwani.

Aliwaonya wafanyabiashara wa dawa za kulevya kuondoka nchini Kenya kabla ya sheria kuwafikia.

“Nimetoa agizo kwamba wote wanaojihusisha na biashara haramu ya dawa za kulevya waondoke humu nchini. Wanafaa kwenda kutafuta mahali pengine pa kufanya hivyo,” Rais Ruto alisema.

Rais pia alitoa wito wa kufungwa kwa mianya na njia zote zinazoshukiwa kutumiwa na wafanyabiashara wa dawa za kulevya kuingiza dawa haramu nchini Kenya.

  • Tags

You can share this post!

Mzee aliyeoa msichana wa miaka 16 ashtakiwa kwa unajisi

Mapenzi yamewatesa sana mastaa hawa, na hivi ndio wameamua...

T L