• Nairobi
  • Last Updated May 22nd, 2024 4:47 PM
Yaibuka Wizara ya Utalii imemumunya mabilioni ya pesa za umma

Yaibuka Wizara ya Utalii imemumunya mabilioni ya pesa za umma

Na MAUREEN ONGALA

KAMATI ya Bunge inayosimamia Utekelezaji, imeibua madai ya ufujaji wa mabilioni ya pesa za umma zilizonuiwa kujenga taasisi ya mafunzo ya utalii ya Ronald Ngala, eneo la Vipingo, Kaunti ya Kilifi.

Hazina ya Utalii, ilikuwa imethibitisha kuwa, kufikia Juni 30, 2020, ilikuwa imetoa Sh4 bilioni kati ya Sh4.9 bilioni zilizohitajika kwa mradi huo.

Hata hivyo, wabunge wanasema imebainika kiasi kikubwa zaidi cha hadi Sh8 bilioni kitahitajika ili kukamilisha ujenzi.

Hazina ya Utalii ni shirika linalokusanya baadhi ya ada za sekta ya utalii, na iko chini ya Wizara ya Utalii inayosimamiwa na Bw Najib Balala.

Kamati hiyo ikisimamiwa na mwenyekiti wake, Bw Moitalel ole Kenta ambaye pia ni Mbunge wa Narok Kaskazini, ilikuwa imezuru eneo la ujenzi wikendi ili kubainisha kama kuna utumizi bora wa fedha za umma.

Walitaka pia kujua sababu za mradi huo kuchelewa kwa karibu miaka saba tangu ulipoanzishwa. Mbunge wa Kilifi Kaskazini, Bw Owen Baya ndiye alikuwa amewasilisha ombi bungeni kutaka kamati hiyo ifanye uchunguzi.

Imedaiwa kuwa, takriban Sh2.9 bilioni zilipotea kupitia kwa ulipaji wa ada ambazo kamati ya bunge inashuku pesa hizo zilienda mifukoni mwa watu binafsi.

Ujenzi wa taasisi hiyo ulikuwa umeanzishwa Aprili 2013 ukitarajiwa kukamilika mwaka wa 2017 kupitia kwa Wizara ya Utalii.

“Mradi huu umetumia takriban Sh8 bilioni ilhali bajeti ilikuwa ni Sh4.9 bilioni, na hadi sasa haujakamilika. Ujenzi umefika asilimia 60 pekee,” akasma Bw ole Kenta.

Alisema ni lazima maafisa wanaosimamia Hazina ya Utalii wawajibike kuhusu suala hilo, na yeyote ambaye atapatikana alipokea pesa haramu atachukuliwa hatua za kisheria.

“Huu ni mradi ambao hautanufaisha Wapwani pekee bali Wakenya wote wanaotegemea utalii. Kama kuna mtu yeyote ambaye alipokea pesa za mlipaushuru kiharamu, lazima wazirudishe kwa Wakenya,” akaongeza.

Mkutano uliofanywa kati ya kamati ya bunge, maafisa wa Bodi ya Hazina ya Utalii, mwanakandarasi (Murji Devraj) na mshauri (Baseline Architects Ltd), ulibainisha kuwa Hazina ya Utalii haikushirikisha afisa kutoka kwa Wizara ya Ujenzi inavyotakikana kisheria.

Ilibainika pia kuwa baadhi ya sehemu zilizohitajika kujengwa kwa msingi wa bajeti ziliachwa nje, kama vile shule ya msingi, na vifaa kama vile gari la huduma za zimamoto.

Mwanzoni, ujenzi huo ulinuiwa kugharimu Sh1.9 bilioni, kisha kiwango kikapanda hadi Sh8.9 bilioni, na baadaye kikapunguzwa hadi Sh4.9 bilioni.

Kamishna wa Kaunti ya Kilifi, Bw Kutswa Olaka ambaye ni mwenyekiti wa kamati ya utekelezaji katika kaunti, alisema kuna wasiwasi kuhusu jinsi ujenzi unachukua muda mrefu kukamilika.

“Tumetembelea eneo la ujenzi karibu mara tano lakini hakuna shughuli zozote zinaendelea. Mojawapo ya mipango ambayo tunawazia ni kuwa kama hakuna hatua zozote zinaendelezwa, tutafute njia mbadala ikiwemo kufanya kituo hiki kiwe chini ya Chuo Kikuu cha Pwani,” akasema.

Bw Baya alilalamika kuwa wakati Bw Balala alipofika mbele ya kamati ya utekelezaji mwaka wa 2017, aliahidi kuwa ujenzi ungekamilika kufikia mwaka wa 2019.

“Pesa nyingi zimetumiwa na hakuna kazi ya kuridhisha imefanywa. Inavyoonekana, huu mradi unacheleweshwa kusudi ili watu wafuje pesa za umma,” akasema.

Akizungumza kwa niaba ya kampuni iliyotoa ushauri kuhusu ujenzi huo, Bw Dominic Mwatanya alisema wametambua sehemu muhimu ambazo zitakamilika kwa miezi 12.

Kaimu Afisa Mkuu Mtendaji wa Bodi ya Hazina ya Utalii, Bw David Mwangi alisema wanatarajia kukamilisha awamu ya kwanza ifikapo Julai 18, 2022.

Kulingana naye, awamu ya pili ambayo itajumuisha ujenzi wa hoteli, itafanywa kwa ushirikiano na shirika la kibinafsi kwa sababu ya changamoto za kifedha serikalini.

  • Tags

You can share this post!

Ondoka Jack Grealish, ingia ?kiungo stadi Emi Buendia!

Tetemeko kubwa lapiga Haiti na kuua watu 1,200