HabariHabari MsetoSiasa

Habari nilitaka Ruto ajiuzulu ni porojo – Matiang'i

August 20th, 2020 1 min read

Na MARY WANGARI

WAZIRI wa Usalama wa Ndani Dkt Fred Matiang’i sasa amewashirikisha mawakili wake kufuatia ripoti kutoka kwa kituo kimoja cha runinga nchini kwamba alimtaka Naibu Rais William Ruto kujiuzulu.

Kupitia taarifa kwa vyombo vya habari mnamo Alhamisi, Agosti 20, 2019, Wizara hiyo ilisema kuwa ripoti zilizotangazwa na kituo hicho cha habari nchini zilikuwa za kupotosha ikizitaja kama “uongo na zenye nia mbaya.”

Aidha, Wizara ilihoji kuwa mawasilisho halisi yangeweza kupatikana katika rekodi za Bunge kwa uthibitishaji.

“Ripoti hiyo ambayo haijathibitishwa ni ya kupotosha kuhusu mawasilisho halisi ambayo yanapatikana kirahisi na kwa umma,” ilisema taarifa hiyo.

Wizara hiyo ilielezea wasiwasi kuwa ripoti kama hizo zinaweza kusababisha uhasama katika tawi la utawala katika serikali.

“Matokeo ya madhara ya ripoti kama hizo za kupotosha yanaweza kusababisha uhasama katika tawi la utawala la serikali,” ilisema.

Isitoshe, Wizara hiyo ilieleza kwamba Dkt Matiang’i sasa ameelekeza suala hilo kwa mawakili wake kujadili hatua itakayofuata.

“Wizara inafahamu vilevile kwamba Waziri ameelekeza suala hilo kwa mawakili wake kwa hatua zaidi,” ilieleza.

Haya yamejiri siku moja tu baada ya Waziri Matiang’i kujiwasilisha mbele ya Kamati ya Seneti kuhusu Usalama mnamo Jumatano, Agosti 19, kwa lengo la kuhojiwa na Seneti.

Matiang’I alihojiwa kuhusiana na kukamatwa kwa maseneta watatu kabla ya kikao cha kujadili kuhusu ugavi wa hela kwa kaunti, ambapo vyombo vya habari vilifungiwa nje na kuzuia kufuatilia kikao hicho.

Maseneta hao Christopher Langat (Bomet), Lelegwe (Samburu) na Cleophas Malala (Kakamega) walikamatwa na kuachiliwa huru baadaye pasipo mashtaka yoyote kuwasilishwa dhidi yao.