Habari za Kitaifa

HABARI ZA HIVI PUNDE: Jaji wa Mahakama Kuu David Majanja aaga dunia

Na FATUMA BARIKI July 10th, 2024 1 min read

JAJI wa Mahakama Kuu David Majanja ameaga dunia akipokea matibabu katika hospitali moja jijini Nairobi.

Jaji Majanja ambaye Mei 2024 alichaguliwa tena kuwakilisha mahakimu na majaji katika Tume ya Huduma za Mahakama (JSC) aliaga dunia akifanyiwa upasuaji, kulingana na duru za familia.

Akithibitisha kifo hicho, Jaji Mkuu Martha Koome alisema Jaji Majanja atakumbukwa kama mhimili mkubwa katika utekelezaji wa Katiba Mpya na katika ujenzi na uendelezi wa taasisi ya mahakama.

“Nina huzuni kubwa kutangaza kifo cha ghafla cha Jaji David Amilcar Shikomera Majanja. Natuma rambirambi zangu na za idara nzima ya mahakama kwa familia yake wakati huu mgumu wa maombolezo,” ikasema taarifa ya Jaji Koome.

Jaji Majanja anakumbukwa kuwa miongoni mwa majaji waliosikiza kesi kuhusu Ushuru wa Nyumba 2023, ambapo waliuharamisha na kuagiza Serikali kuwazia upya jinsi ushuru huo unavyoweza kutekelezwa kisheria.