Habari za Kitaifa

HABARI ZA HIVI PUNDE: Wahuni wangali wanahangaisha polisi wakitaka kupora supamaketi Karatina


WAANDAMANAJI wanaoshukiwa kuwa wahuni wangali wanakabiliana na polisi mjini Karatina, wakitegea kuvunja duka la supamaketi ili kupora.

Kufikia saa mbili kasorobo usiku Jumanne, Julai 2, 2024, vikosi vya polisi vilikuwa vinakabiliana na makundi ya vijana waliokataa kuondoka licha ya kwamba maandamano yalishakwisha katika miji mingi kufikia jioni.

Takriban watu saba wakiwemo polisi wawili wamejeruhiwa katika makabiliano ambayo yalikuwa yanaendelea kufikia wakati wa kuandika taarifa hii.

Supamaketi iliyolengwa ni Mathai inayohusishwa na mwanasiasa mmoja Nyeri, kaunti ambayo ni nyumbani kwa Naibu Rais Rigathi Gachagua.

Duka hilo lililengwa mchana kutwa huku magenge ya vijana yakikimbizana na polisi bila kukoma. Wakati fulani, jioni, vitoa machozi viliishia polisi, jambo lililotia nguvu magenge hayo kabla ya polisi kupata vikosi vya ziada kuendelea na mapambano.