• Nairobi
  • Last Updated April 20th, 2024 5:23 PM
Ajabu watu 2 pekee wakihudhuria sherehe ya Leba Dei Eldoret   

Ajabu watu 2 pekee wakihudhuria sherehe ya Leba Dei Eldoret  

Na TITUS OMINDE

NI dhahiri kuwa hakukuwa na sherehe za siku ya wafanyikazi katika Kaunti ya Uasin Gishu, nyumbani kwa Rais William Ruto.

Hakukuwa na watu waliojitokeza kushiriki katika sherehe za Sikukuu ya Wafanyakazi ambazo zilipaswa kufanywa katika uwanja wa Shule ya Msingi ya Eldoret Central, hafla ya mwaka huu.

Eneo hilo kubwa lilikuwa na maafisa wawili pekee kutoka Muungano wa Kutetea WafanyakaziNchini (COTU).

Wawili hao ni pamoja na Mwakilishi wa COTU Kaskazini mwa Rift Valley Peter Odima pamoja na naibu wake Rodgers Ombati wakiwa na nakala za hotuba kutoka kwa katibu mkuu wa COTU Bw Francis Atwoli.

Bw Odima alishutumu uongozi wa kaunti ukiongozwa na gavana Jonathan Bii kwa kukosa kushirikiana na chama cha wafanyakazi kuandaa sherehe hiyo.

Bw Odima alisema kaunti hiyo iliahidi kutoa mahema, viti na mahitaji mengine ili kuhakikisha sherehe zinafaulu lakini katibu wa kaunti hiyo alinyamaza dakika za mwisho akiwaacha viongozi wakiwa wamekwama.

“Kufikia jana usiku katibu wa kaunti alikuwa amekubali kutuunga mkono jinsi ilivyokuwa wakati wa sherehe za awali. Inasikitisha kwamba aliamua kutuangusha dakika za mwisho,” akasema Bw Odima.

Bw Odima alilazimika kumshauri Kamishna wa Kaunti kutoshiriki hotuba ya rais kwa vile hakukuwa na umati wa kuhutubia.

Uwanja mtupu wa Shule ya Msingi ya Central mjini Eldoret ambako kungefanyika sherehe ya leba dei. Picha / Titus Ominde

Alisema kuwa alishangaa kufika katika uwanja ukiwa mtupu bila hema na viti kutoka kwa kaunti kama alivyoahidiwa.

“Nililazimika kumwita kamishna wetu wa kaunti asije uwanjani kwa sababu hakukuwa na kiti hata kimoja. Hii ni mara ya kwanza tunaaibishwa na utawala wa gavana Jonathan Bii,” alisema Bw Odima.

Alilazimika kusambaza nakala za hotuba ya katibu mkuu wa COTU kwa wanahabari wachache waliokuwa wamefika kuangazia tukio hilo.

Bw Odima alisikitika kuwa bosi wake wa COTU alimtumia tu nakala za hotuba hiyo bila kutoa ufadhili kwa sherehe husika.

“Hata chama changu hakijafanya lolote kutuunga mkono kuadhimisha siku ya wafanyikazi katika eneo hili. Jambo la pekee walilofanya ni kutuma vijitabu vya hotuba bila kujua mipango ya sherehe,” alisema Bw Odima.

Alitoa changamoto kwa utawala wa gavana Bii kuiga mtangulizi wake Jackson Mandago ambaye alimsifu kwa kuunga mkono hafla za wafanyikazi katika kaunti katika kipindi chake chote.

“Namsifu Bw Mandago kwa uungwaji mkono aliokuwa akitupatia wakati wa uongozi wake. Ombi langu ni kwamba mrithi wake aige vivyo hivyo,” akasema Bw Odima.

Bw Peter Odima na mwenzake Rodgers Ombati wakihitubi wanahabari baada ya sherehe hiyo kukosa wananchi kutokana na mipango duni. Picha / Titus Ominde

 

  • Tags

You can share this post!

Leba Dei 2023: Askofu asuta Raila Odinga kupitia maombi

Ajabu watu 2 pekee wakihudhuria sherehe ya Leba Dei Eldoret...

T L