• Nairobi
  • Last Updated November 28th, 2023 7:53 PM
Askari wanavyohamasishwa Migori kupunguza visa vya unyanyasaji wa kijinsia 

Askari wanavyohamasishwa Migori kupunguza visa vya unyanyasaji wa kijinsia 

NA WYCLIFFE NYABERI 

ZAIDI ya maafisa 30 wa polisi katika Kaunti ya Migori wamenufaika na mafunzo yanayolenga kupunguza visa vya Unyanyasaji wa Kijinsia (GBV), ambavyo vimekithiri katika gatuzi hilo.

Mafunzo hayo yaliyofadhiliwa na Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya Kupambana na Dawa za Kulevya na Uhalifu (UNODC) na kufanyika katika mji wa Migori, yalishuhudia maafisa hao kuelimishwa jinsi ya kuchunguza, kushtaki na kuzuia kesi za dhuluma za kijinsia ambazo hutokea sana wakati wa likizo ndefu baada ya shule kufungwa.

Paul Ndambuki, mmoja wa maafisa walionufaika na mpango huo alisema wamepokea ujuzi zaidi utakaowawezesha kuzuia maovu hayo.

Aliongeza kuwa takwimu zinaonyesha Migori ni miongoni mwa kaunti ambazo zinaongoza kwa visa vya GBV.

Kwa mfano katika kisa kimoja cha Desemba 2022, maafisa wa polisi waliwaokoa wasichana watano waliokuwa kwenye hatari ya kukeketwa katika kijiji cha Ntunyigi, Wadi ya Bukira Mashariki, Kaunti Ndogo ya Kuria Magharibi.

Wanne kati yao walikuwa wanafunzi wa darasa la sita.

Serikali ya Kaunti ya Migori ilipokuwa ikizindua hamasisho la kukomesha dhulma za kijinsia mwaka jana, 2022, maafisa kutoka Idara ya Jinsia, Utamaduni na Masuala ya Vijana walisema kuwa wanafanya kazi bila kuchoka ili kutokomeza visa vya GBV gatuzini.

“Kama idara pia, tunahakikisha kwamba mila ambayo inaweza kuhatarisha mtoto wa kike inakomeshwa huku tukitetea njia zingine mbadala,” Bi Lilian Gomo kutoka idara hiyo husika alisema wakati huo.

Pia aliongeza kwamba wanaelimisha jamii kufuata tamaduni ambazo hazimuumizi mtoto wa kike.

Mbali na ukeketaji, dhulma zingine ambazo zimetajwa kujitokeza Migori ni unyanyapaa hasa kwa wagonjwa wa Saratani ya mlango wa kizazi kwani baadhi waathiriwa wamefukuzwa kwenye nyumba zao za ndoa huku wengine wakitelekezwa na watu wa karibu wa familia zao kwa dhana potovu kuwa wamerogwa.

Washiriki wengine waliohudhuria hamasisho hilo, walisema mafunzo hayo yatawafaa sana na kuahidi kufunza wenzao ambao hawakupata fursa ya kuhudhuria kikao hicho.

Waliwashukuru waandalizi wa mafunzo hayo huku wakiwataka wawe wakiyafanya mara kwa mara, wakisema yanajiri wakati ambapo wanaharakati wa kijinsia wanazidi kutoa wito wa kufanya kazi pamoja ili kupunguza dhulma kama ukeketaji.

 

  • Tags

You can share this post!

Wahuni waliokuwa wakikeketa wasichana Pokot Magharibi...

Mbinu maalum anayotumia mfugaji kupata malisho eneo kame...

T L