• Nairobi
  • Last Updated October 2nd, 2023 7:00 AM
Askari wasababisha vifo vya watu 4 wakikimbizana na chang’aa   

Askari wasababisha vifo vya watu 4 wakikimbizana na chang’aa  

 

NA JESSE CHENGE 

WATU wanne wamepoteza maisha eneo la Chwele, Bungoma katika ajali iliyohusisha gari la polisi na pikipiki.

Kulingana na walioshuhudia mkasa huo, gari la askari lilikuwa likikimbiza mwendesha pikipiki aliyekuwa akisafirisha chang’aa – pombe haramu kuelekea Kimilili.

Mhudumu huyo aligongana ana kwa ana na mwenzake wa bodaboda, hali ya mkanganyiko iliyosababisha maafa ya watu watatu papo hapo.

‘Tumekerwa sana na kitendo hiki ambapo polisi wamesababisha vifo vya watu wetu, naomba mamlaka zinazohusika zichukue hatua, zifanye uchunguzi na kuadhibu kisheria polisi waliohusika,” Abiud Wekesa, mmoja wa walioshuhudia akaambia Taifa Leo.

Mtu mwingine, alipofariki wakati akiendelea kupokea matibabu katika Hospitali ya Chwele na kufikisha idadi ya jumla ya waliofariki kutokana na utepetevu wa askari kuwa nne.

Ajali hiyo aidha ilikera wakazi na wafanyabiashara Chwele, kilele kikiwa kuchipuka makabiliana makali kati yao na polisi.


Raia Chwele, wakiandamana na kufunga barabara kufuatia ajali iliyohusisha gari la polisi na kusababisha maafa ya watu wanne. Picha / JESSE CHENGE

Wakilalamikia utepetevu wa askari, wafanyabaishara Chwele wametishia kuandaa maandamano na kuyapeleka katika Kituo cha Polisi cha Chwele.

Wamewataka viongozi wa kisiasa Bungoma na pia wa kiusalama kuingilia kati kusaidia kuchukulia hatua kali na za kisheria askari waliohusika.

Kwa upande wake mwakilishi wadi wa Mukuyuni (MCA), Meshack Museveni alilaani kisa hicho akilaumu polisi kwa utepetevu na uzembe.

“Kazi ya polisi sio kufukuza wanaosafirisha pombe haramu, bali ni kulinda watu na mali zao. Isitoshe, mtu anapokosa mahakama zipo, afunguliwe mashtaka,” Bw Museveni alisema.

Baadhi ya askari Kituo cha Polisi Chwele wametajwa kusalia humo kwa muda mrefu, MCA Museveni akipendekeza wahamishwe.

Miili ya walioangamia katika ajali hiyo ilipelekwa katika hifadhi ya maiti ya Hospitali ya Kaunti, Bungoma upasuaji ukisubiriwa kufanyika.

  • Tags

You can share this post!

Museveni achapa kazi licha ya kupimwa na kupatikana ana...

NiE: Mkataba wa NMG na KIWASCO unavyopiga jeki elimu Kisumu

T L