• Nairobi
  • Last Updated April 24th, 2024 1:05 PM
Awali ilikuwa milio ya risasi na magaidi Lamu, sasa ni unyunyu na starehe

Awali ilikuwa milio ya risasi na magaidi Lamu, sasa ni unyunyu na starehe

NA KALUME KAZUNGU

MIAKA kumi iliyopita, Lamu lilikuwa eneo la kutisha na lililoogopwa na wengi waliotamani kulifikia, wakiwemo watalii na wageni wengine.

Woga huo ulichangiwa hasa na mashambulio ya kila mara yaliyokuwa yakitekelezwa na wapiganaji wa Al-Shabaab kutoka nchi jirani ya Somalia.

Magaidi hao walikuwa wakivuka kuingia Lamu kwa kutumia msitu mkubwa wa Boni ambao pia kwa miaka mingi umekuwa maficho na ngome inayotumiwa na Al-Shabaab kuendeleza mashambulio kwenye vijiji mbalimbali vya Lamu na katika maeneo mengine nchini Kenya.

Shambulio kubwa zaidi la Al-Shabaab lililotekelezwa Lamu na kutia watu – wenyeji, wageni na watalii – woga ni lile la usiku wa Juni 15, 2014 mjini Mpeketoni na Kibaoni, ambapo wanaume wapatao 100 waliuawa, magari na nyumba zaidi ya 50 zikiteketezwa moto na maaidi hao.

Baadaye, miji ya Witu, Hindi, vijiji vya msitu wa Boni, ikiwemo Milimani, Basuba, Mararani, Mangai, Kiangwe na Bodhei, pia vikaanza kushuhudia msururu wa mashambulio ya Al-Shabaab, serikali ikilazimika kuagiza taasisi za elimu na afya zifungwe.

Kushoto na mwenye nguo za kawaida ni Naibu Gavana wa Lamu Raphael Munyua na Mbunge wa Lamu Mashariki Ruweida Obbo (mwenye baibui), Meja-Jenerali Juma Mwinyikai na maafisa wengine wa KDF wakati walipozuru kijiji cha Mararani ndani ya Msitu wa Boni. Ushirikiano uliopo kati ya raia na jeshi umesaidia kuleta usalama msituni Boni na Lamu kwa ujumla. PICHA | KALUME KAZUNGU

Mnamo Septemba 2015 wakati Al-Shabaab walikuwa wanashambulia Lamu usiku na mchana, serikali kuu ilizindua operesheni maalum kwa jina ‘Linda Boni’ dhamira kuu ikiwa ni kuwasaka na kuwamaliza  au kuwafurusha magaidi hao walioaminika kujificha ndani ya msitu wa Boni.

Licha ya operesheni kuendelezwa, hali haikubadilika kiurahisi kwani Al-Shabaab mara nyingi bado walikuwa wakikwepa mitego ya wanajeshi (KDF), polisi na vikosi vingine vya usalama vinavyoendeleza operesheni hiyo, kuvuka na kuingia vijiji vya Lamu kutekeleza mauaji na uharibifu wa mali.

Huku mapigano ya moja kwa moja kwa kutumia mtutu wa bunduki kwa walinda usalama dhidi ya Al-Shabaab yakiendelezwa msituni Boni, idara ya usalama iliona vyema kubadili mifumo au mbinu mbadala za kufaulisha vita dhidi ya Al-Shabaab Lamu na hata kuhakikisha tatizo hilo linaangamizwa kabisa.

Cha kutia moyo zaidi ni kwamba karibu mwongo mmoja sasa umepita ambapo Lamu imepiga hatua kubwa kiusalama kwani amani na utulivu unaendelea kudumishwa.

Taifa Leo ilizama ndani kuchambua baadhi ya mifumo ambayo walinda usalama, hasa wale wanaohudumia msitu wa Boni na maeneo mengine ya Lamu yaliyoshuhudia mashambulio ya Al-Shabaab wamekuwa wakiitumia kushinda vita dhidi ya ugaidi.

Katika mahojiano ya awali na Kamanda wa Kikosi cha Ukanda wa Mashariki Jeshini (KDF), Meja-Jenerali, Juma Mwinyikai wakati wa ziara yake kwenye vijiji vya msitu wa Boni, alifichua kuwa ushirikiano waliodumisha na kuunawirisha kati yao na raia wa vijiji vya msituni umechangia pakubwa kufaulishwa kwa vita dhidi ya Al-Shabaab.

Bw Mwinyikai alikiri kuwa KDF, polisi na wananchi kwenye eneo hilo la operesheni miaka ya hivi punde wamekuwa wakichukuliana kama ndugu na dada, hatua aliyoitaja imerahisisha upashanaji habari kati ya raia na maafisa wa usalama kumhusu adui.

“Badala ya kuelekeza fikra zetu zote kumkabili adui kwa bunduki miaka yote, pia tuliafikiana kuupalilia uhusiano wetu na jamii. Kuna uhusiano mzuri kwa sasa. Hili limeondoa woga wa raia wanapowaona KDF. Ushirikiano uliopo kati ya pande hizi mbili umesaidia pakubwa kupashana taarifa kuhusu Al-Shabaab, hivyo kukabili na kuyadhibiti mashambulio yanayopangwa na adui mapema, kuzuia maafa na uharibifu wa mali. Twatarajia hali ikiendelea hivi zogo la Al-Shabaab liangamizwe kabisa ili tupate Lamu na nchi salama,” akasema Bw Mwinyikai.

Walinda usalama wanaohudumu kwenye msitu wa Boni pia wamekuwa mstari wa mbele kuwafadhili vijana wasome ili hatimaye watimize malengo yao.

Mapema Februari 2023, KDF waliwasafirisha kwa helikopta vijana watatu waliokuwa wamepasi Mtihani wa Kitaifa wa Darasa Nanedarasa  (KCPE) kutoka msitu wa Boni hadi kwenye shule ya upili ya jeshi ya Moi Forces Academy jijini Nairobi ambako wanawafadhili kimasomo.

Vijana hao ni Nathaniel Ushindi Chanzera,17, Ryan Karisa,16, na Ali Mohamed,15.

Isitoshe, walimu zaidi ya 30 wanaofundisha kwenye shule za msitu wa Boni pia wamekuwa wakisaidiwa kiusafiri kupitia ndege ya KDF kila mara wanapofunga shule kuelekea nyumbani n ahata shule zinapofungwa na wanapotaka kurejea shuleni kufundisha.

Ili kuendeleza uhusiano huo mwema na jamii, walinda usalama pia wamekuwa wakiwahifadhi au kuwapa makao walimu wanaofundisha msitu wa Boni kwenye kambi zao.  Januari mwaka huu, KDF waliwasafirisha kwa ndege walimu 25 waliokuwa wakiripoti kwenye shule zao za msitu wa Boni baada ya muhula wa kwanza kuanza.

Walimu hao walikuwa wa shule za Milimani, Basuba, Mangai, Mararani na Kiangwe.

Kulingana na Kamanda Msimamizi wa Operesheni ya Amani Msituni Boni, Kanali Joel Tanui, walinda usalama pia wamekuwa wakisaidia wananchi wa msitu wa Boni kwa kuwasafirisha kwa ndege hospitalini punde dharura inapotokea.

“Pia tumejenga shule, kuchimbia wananchi visima, kutoa kambi za bure za matibabu, na kusambaza maji vijijini. Yote haya tunayafanya kudumisha uhusiano mwema kati yetu na raia. Hili limesaidia sana katika vita dhidi ya Al-Shabaab eneo hili kwani raia wako huru kufahamisha vitengo vya usalama iwapo kuna adui au tukio wanalolishuku kuwa kero kwa usalama kinyume na ilivyokuwa awali,” akasema Bw Tanui.

Hamasa za kila mara kwa umma, hasa vijana kuhusiana na mapambano dhidi ya itikadi kali na ugaidi pia zimeimarishwa miaka ya hivi punde hali ambayo imepunguza idadi ya wanaoraiwa kupokea mafunzo ya kigaidi na kisha kuvuka Somalia kujiunga na Al-Shabaab.

Baadhi ya raia Lamu wakiwa na viongozi wao. PICHA | KALUME KAZUNGU

Kusajiliwa kwa vijana, hasa Waboni kujiunga na jeshi pia ni hatua kubwa inayoendelea kufaulisha vita dhidi ya uaidi Lamu.

Kulingana na Naibu Kamishna wa Lamu, Philip Oloo, jamii kwa sasa inajiisi kuwa kiungo muhimu katika kudhibiti usalama wa nchi.

Bw Oloo alisema ili kuvunjilia mbali daraja au pengo lililokuwepo kati ya raia na walinda usalama, mechi mbalimbali za kandanda zinazojumuisha walinda usalama na raia zimekuwa zikiandaliwa kwenye maeneo mbalimbali ya Lamu kila mara.

“Ukilinganisha miaka kati ya 2014, 2018 na sasa, utapata tumepiga hatua kubwa kiusalama. Lamu ina amani na utulivu. Polisi, KDF na raia pia wanatagusana na kushikamana vyema. Hilo limerahisisha vita dhidi ya Al-Shabaab. Na hii ndiyo sababu ninasisitiza walinda usalama wetu kuwajumuisha raia kwenye operesheni na doria zao za usalama ili kumkabili na kumshinda huyu adui wetu sote ambaye ni mmoja-Al-Shabaab,” akasema Bw Oloo.

Maafisa wa usalama pia wamekuwa wakiwashirikisha viongozi, hasa wanasiasa kwenye mijadala ya kuleta uwiano na utangamano na kuwashauri kuepuka kuingiza siasa kwenye suala la usalama.

Kufunguliwa na kuendelezwa kwa miradi mikubwa ya maendeleo ya kitaifa kama vile barabara ya Lamu-Witu-Garsen, bandari ya Lamu na miradi mingine tanzu ya uchukuzi wa Kenya, Ethiopia na Kusini mwa Sudan (Lapsset) pia ni changizo kuu ya kudhibitiwa kwa usalama wa Lamu.

Serikali ya kitaifa na kaunti pia zimekuwa mstari wa mbele kujadili na kutatua migogoro ya ardhi, ajira na dawa za kulevya miongoni mwa vijana na jamii kwa ujumla, vigezo vinavyoweza kutumiwa vibaya na maadui kuwarai na kuwapa vijana mafunzo ya itikadi kali na kisha kuwafanya kujiunga na makundi ya uhalifu.

Juma lililopita wakati wa maadhimisho ya Sikukuu ya Madaraka, Gavana wa Lamu, Issa Timamy aliimiminia sifa kochokocho serikali kuu, hasa idara ya usalama kwa kuhakikisha amani na utulivu unarejeshwa na kudumishwa kwenye eneo hilo.

“Nawapongeza maafisa wetu wa usalama, hasa wale walioko msitu wa Boni kwa kukabiliana na Al-Shabaab na kuangamiza kabisa utovu wa usalama eneo hili. Isitoshe, wao wamekuwa wakisaidia watu wetu wanapohitaji huduma za matibabu kwa kuwapeperusha kwa ndege zao kuwafikisha hospitalini. Ningesihi wananchi wangu kuendelea kudumisha ushirikiano huo na walinda usalama wetu ili tufurahie amani na utulivu kwa maendeleo ya kaunti yetu,” akasema Bw Timamy.

  • Tags

You can share this post!

Sapoti ya Wakenya iko juu, mamake Jeff Mwathi asema akiomba...

Sabina Chege ajeruhiwa katika fujo zilizozuka Bungeni mnamo...

T L