• Nairobi
  • Last Updated April 19th, 2024 8:55 PM
Bangi imeharibu ‘transfoma’ za vijana wengi Lamu – polisi

Bangi imeharibu ‘transfoma’ za vijana wengi Lamu – polisi

NA KALUME KAZUNGU

IDARA ya polisi tarafa ya Mpeketoni, Kaunti ya Lamu imelalamika kwamba inapokea ripoti nyingi za mizozo ya wanandoa inayoaminika kuchangiwa na uvutaji bangi, utafunaji wa muguka na matumizi ya dawa za kulevya.

Afisa Msimamizi wa Kituo cha Polisi cha Mpeketoni, Richard Ngunjiri anasema uvutaji bangi unaoshuhudiwa kwa wingi, hasa Mpeketoni, Baharini na viungani mwake, umelemaza nguvu za kiume miongoni mwa vijana wengi, hivyo kuwafanya wake wa baadhi yao kulalamika na migogoro kuongezeka kwa familia.

Bw Ngunjiri anasema ndoa nyingi pia zimeshuhudiwa zikivunjika eneo hilo kutokana na ‘transfoma’ za wanaume kufishwa na uvutaji bangi na matumizi ya mihadarati kwa ujumla.

Anasema baadhi ya wanaume wamekuwa wakifurika kwenye maduka ya dawa kutafuta mbinu mbadala za kuwasisimua chumbani ikiwemo kuingilia ununuzi na matumizi ya tembe za kuongeza nguvu za kiume ‘viagra.’

Afisa huyo anasema matumizi ya bangi na dawa za kulevya kwa jumla pia yamewasukuma wanaume wengi kwenye misongo ya mawazo, hasa punde wanapokosa kukimu shughuli kitandani, hivyo kuishia kujitoa uhai.

“Inasikitisha kwamba vijana wa kati ya umri wa miaka 18 na 23 tayari transfoma zao hazifanyi kazi. Wake wa baadhi yao wamekuwa wakilalamika, kukosana na hata kuishia kuwasilisha migogoro yao kwa polisi. Haya yote yanasababishwa na bangi nyingi inayovutwa na hawa vijana. Unapata wengine wanapokosa kuwakimu wake zao kitandani wanaleta vurugu, kukosana na wake zao na kisha wanaishia kujiua. Ripoti za watu kujitia kitanzi na kufariki zimekithiri sana hapa Baharini na tarafa ya Mpeketoni kwa ujumla. Lazima tujiepushe na uvutaji bangi na matumizi ya mihadarati,” akasema Bw Ngunjiri.

Mkuu huyo wa polisi anawashauri vijana washiriki michezo kama kandanda, voliboli, mbio na mazoezi mengine kila wanapopata mwanya huru badala ya kukimbilia kujitosa kwenye lindi la dawa za kulevya zinazodhoofisha afya zao na kuchangia migogoro na kusambaratika kwa familia.

“Mpeketoni tumebarikiwa kuwa na viwanja vingi vya michezo. Badala ya vijana kupotelea kwa kutafuna muguka, kuvuta bangi na kuharibu ndoa ambapo watoto wanaachwa wakiteseka, wajikaze kushiriki mazoezi, hasa kandanda na michezo mingine kuimarisha afya na miili yao,” akasema Bw Ngunjiri.

Lakini ni hivi majuzi tu ambapo wazee wa vijiji vya Mpeketoni na Baharini walijitokeza kulalamikia ongezeko la visa vya wasichana wa shule kutungwa mimba kiholela, wahudumu wa bodaboda, hasa wale wanotumia dawa za kulevya, ikiwemo bangi wakitajwa kuchangia uozo huo.

“Mtu punde anapovuta bangi anamuona mtoto wa umri wa miaka 12 au 16 kuwa mwanamke tosha wa kushiriki naye ngono na kuishia kumpachika mimba. Baadaye mtoto huyo anaachwa kuteseka ndoto yake ya masomo ikitiwa doa jeusi hivyo. Idara ya usalama ifuatilie suala hili kwa karibu na kulikomesha,” akasema mzee wa kijiji cha Baharini Bw Simon Mwangi.

  • Tags

You can share this post!

Mwanamume auawa na umati akidaiwa kuiba mihogo  

Azimio wapendekeza Mwenje awe naibu kiranja wa wachache...

T L