• Nairobi
  • Last Updated February 25th, 2024 10:30 AM
El Nino: Hofu nyanda za juu Pokot Magharibi mmomonyoko wa udongo ukitishia wakazi 

El Nino: Hofu nyanda za juu Pokot Magharibi mmomonyoko wa udongo ukitishia wakazi 

NA OSCAR KAKAI

WASIWASI umekumba wakazi wa nyanda za juu Kaunti ya Pokot Magharibi, wakihofia kuporomokewa na udongo kufuatia mvua ya El Nino inayoendelea kushuhudiwa.  

Maeneo yalioathirika zaidi ni ya miinuko ya eneo pana la Lelan, Kaunti Ndogo ya Pokot Kusini na Pokot ya Kati.

Aidha, maeneo hayo yanazidi kupokea mvua kubwa hali ambayo imeathiri wakazi na mazao shambani.

Isitoshe, ukungu umeshamiri na barabara hazipitiki nyingi zikiishia kufurika.

Mwaka wa 2019 na 2020, zaidi ya watu 60 walipoteza maisha, mali kuharibika, na wakazi wasiopungua 1, 500 kuhama makwao maeneo ya Nyarkulian, Parua, Muino na Chesegon baada ya mafuriko na maporomoko ya udongo kutokea.

Maeneo hayo pia yameandikisha visa vya radi kupiga watu na mifugo.

Wakazi wanasema kuwa udongo kwenye milima umekuwa mwepesi, na unaanza kumomonyoka hivyo basi wakilazimika kuhama.

“Kwa sasa tunaishi kwa hofu. Barabara za Tapach – Nyarkulian, Sondany –Kacheprikong hazipitiki. Tuna wasiwasi milima huenda ikaporomoka wakati wowote,” alisema Michael Siwareng mkazi wa eneo la Kacheprikong.

Bernard Chepkub, mkazi wa eneo la Tapach alilalamikia ukungu kuathiri eneo hilo.

“Kwa wiki moja sasa, huwezi kuona mbali. Tunaomba serikali itusaidie kutatua changamoto zinazotuzingira,” alisema.

Seneta wa Kaunti hiyo, Julius Murgor pamoja na Katibu katika Wizara ya Ujenzi, Joel Arumonyang ambao wako katika eneo la Tapach kutathimini hali waliitaka serikali kuu na ya kaunti kuunda na kukarabati barabara eneo hilo ili wakazi waweze kusafirisha mazao yao vyema.

Bw Arumonyang alisema kuwa wanahamasisha wakazi dhidi ya athari za Elnino na maporomoko ya ardhi.

“Tunataka wakazi kupiga ripoti kuhusiana na hatari yoyote,” alisema.

Waziri wa Huduma za Umma katika afisi ya Gavana Pokot Magharibi, Martin Lotee aliitaka serikali kuweka lami kwenye barabara eneo hilo ili kusaidia wakulima kusafirisha mazao yao sokoni.

“Wakulima wanakadiria hasara kubwa kutokana na mvua ambayo inanyesha,” alisema.

Alisema kuwa serikali ya kaunti imetenga fedha kukabiliana na majanga ya dharura.

  • Tags

You can share this post!

Hatimaye Serikali yatoa Sh10 bilioni kukabili athari za El...

Simba jike atishia kuangusha Ripoti ya Kamati ya Maridhiano...

T L