• Nairobi
  • Last Updated April 17th, 2024 6:55 PM
El Nino: Mbunge alalamikia ubaguzi katika usambazaji wa chakula Mombasa

El Nino: Mbunge alalamikia ubaguzi katika usambazaji wa chakula Mombasa

NA WINNIE ATIENO

MBUNGE wa Likoni Bi Mishi Mboko ameishutumu serikali kuu akidai inasambaza chakula cha msaada kwa waathiriwa wa mafuriko huko Mombasa kwa ubaguzi.

Hii ni baada ya serikali kuu kuendelea kusambaza chakula cha msaada kupitia Mbunge wa Nyali Bw Mohammed Ali badala ya Gavana wa Mombasa Bw Abdulswamad Nassir.

Bw Ali ambaye ndiye mbunge aliyechagulia kupitia chama tawala cha UDA, amekuwa akisambaza chakula mitaani Mombasa hasa mitaa ambayo wakazi waliathirika na mafuriko.

Hata hivyo, Bi Mboko alisema ni wajibu wa serikali kuu kusambaza chakula hicho kwa kushirikiana na Gavana Nassir ambaye ndiye mwakilishi wa wakazi wa Mombasa katika serikali kuu.

Bi Mboko alisema serikali kuu ilisambaza chakula cha msaada kwa waathiriwa wa janga la mafuriko kupitia mbunge.

“Sisi kama viongozi tumeona suala hili limechukuliwa kisiasa. Sababu kama desturi, serikali kuu zilizopita zimekuwa zikigawa chakula cha msaada wakati wa majanga kama haya kupitia kwa kamishna wa kaunti, manaibu wao na machifu lakini safari hii tulishangaa,” alilalamika Bi Mboko.

Badala yake, mbunge huyo alisema chakula hicho kinafanyiwa siasa.

“Si sawa kufanyia chakula siasa. Kiongozi wa kisiasa hafai kutumia chakula hicho kisiasa na hata kubagua wengine. Isitoshe, watu wengi walikosa hicho chakula, na hakukuwa na mpangilio kisawasawa,” aliongeza mwandani huyo wa Bw Nassir.

Alisema watu ambao wamekuwa wakisambaza chakula hicho cha msaada, wamekuwa wakimponda Bw Nassir.

Bw Ali amekuwa akisambaza chakula cha msaada katika mitaa kadha wa kadha.

Alisema alimwambia Rais William Ruto asaidie waathiriwa wa janga la mafuriko na akakabidhiwa vyakula vya msaada azunguke Mombasa akiisambaza.

“Kuna dhambi nikileta chakula? Nimeleta chakula hasa kwa wale ambao wamesahaulika. Lakini ninataka kumwambia Gavana wa Mombasa, awache kwenda mahotelini kula kaimati, aje asaidie watu,” alisema Bw Ali siku tano zilizopita, akizungumza eneo la Makande.

Vile vile, mbunge huyo ambaye ni mwandani wa Dkt Ruto alishtumu wakazi kwa kujenga kwenye maeneo ya ziwa na kuathiri maisha yao wakati wa mafuriko.

Hata hivyo, alisema serikali ya kaunti ilijizatiti na kuwahamishia sehemu zingine.

“Sehemu nyingi Kisauni zinazoshuhudia mafuriko ni kule ziwani, lakini watu wakaenda kujenga. Tumewasaidia na chakula, dawa, na neti za mbu. Wale ambao nyumba zimeanguka tunashirikiana na Gavana kuwasaida kununua mabati,” alisema Bi Mboko.

 

  • Tags

You can share this post!

Hapa vitenge na jezi tu: Sababu za Mkuu wa Utumishi wa Umma...

Wadudu wa ‘Nairobi fly’ wanavyohangaisha Wakenya msimu...

T L