NA TITUS OMINDE
WANAHARAKATI kutetea haki za kibinadamu, wakiongozwa na Haki Africa, wameitaka Tume ya Huduma za Polisi Nchini (NPSC) kusimamisha kazi askari wa gereza la Eldoret wanaohusishwa na kifo cha mababusu kwenye jela.
Hussein Khalif, Afisa Mkuu Mtendaji, Haki Africa, amemshinikiza Waziri wa Usalama wa Ndani na Mikakati ya Setikali, Kithure Kindiki kuingilia kati na kuhakikisha maafisa wanaotuhumiwa kusababbisha kifo cha mabusu aliyeuawa katika hali isiyoeleweka Eldoret GK wamechukuliwa hatua za kinidhamu.
Afisa huyo pia, amemtaka Prof Kindiki kuhakikisha haki kwa familia ya marehemu mahabusu Oliver Ochieng, 28 imepatikana.
Akizungumza na wanahabari katika Hospitali ya mafunzo na Rufaa ya Moi baada ya kushuhudia uchunguzi wa upasuaji wa marehemu, Bw Khalif alisema inatia wasiwasi kutambua kwamba marehemu alifariki katika mazingira ya kutatanisha akiwa mikononi mwa maafisa wa magereza.
Afisa huyo alidai kuwa Bw Ochieng aliteswa kabla ya kuuawa kikatili, akibainisha kuwa mikono yake ilikuwa na makovu mapya yaliyoashiria kuwa alikuwa akijikinga dhidi ya mashambulizi.
Pia alisema kuwa ripoti ya uchunguzi wa maiti ilionyesha kuwa marehemu alikosa Oksijeni kabla kukumbatana na mauti akiwa gerezani.
“Tunaomba kusimamishwa kazi mara moja kwa maafisa wanaolaumiwa kwa mauaji ya kikatili ya mshukiwa aliyeuawa huku uchunguzi ukiendelea.
“Mshukiwa aliyekuwa chini ya ulinzi wao, alikuwa akisubiri kuachiliwa na mahakama kutokana na ukosefu wa ushahidi katika kesi ambayo alikuwa anakabiliwa na mashtaka ya wizi wa kutumia nguvu,” alisema Khalif.
Wakati huohuo, Bw Kimutai Kurui kutoka Centre Against Torture aliiomba serikali kuweka kamera za CCTV katika magereza yote ili kusaidia kufuatilia kile kinachotokea kwenye magereza kote nchini.
“Ni jambo la busara kwa mamlaka inayohusika kuhakikisha kuwa vituo vyote vya kurekebisha tabia nchini vimewekwa kamera za CCTV ili kuepusha visa vingi vya utesaji na mauaji ambayo hutokea magerezani,” alisema Kurui.
Alisema wamepokea malalamiko mengi kutoka kwa wahanga wa kuteswa na kupigwa na maafisa wa magereza North Rift, akionya kuwa suala hilo lisiposhughulikiwa haraka iwezekanavyo, watuhumiwa wengi zaidi wataendelea kupoteza maisha wakiwa gerezani.
Bw Ochieng alidaiwa kuuawa kwa kupigwa risasi na maafisa wa wasimamizi wa gereza ambao bado hawajajulikana.
Inadaiwa kuwa marehemu alikuwa amekaidi maagizo ya maafisa hao ya kuketi katika kundi la wafungwa wengine kwa ajili ya kuhesabiwa, jambo lililozua makabiliano.
Kwa mujibu wa maelezo ya mahabusu mwenza, ambaye aliomba kubana jina lake kwa sababu za kuisalama alisema kuwa Ochieng alikaidi maagizo hayo na badala yake alitembea hadi mahali pa faragha katika gereza hilo ili kusali.
“Bw Ochieng alikuwa mfungwa aliyebadilika, mcha Mungu na mtiifu ambaye alijitolea kusali kila asubuhi, wakati wa chakula cha mchana na jioni. Hakustahili kufa namna hiyo,” alisema mwenzake.