• Nairobi
  • Last Updated November 28th, 2023 7:53 PM
Huzuni mtangazaji nyota akijitia kitanzi

Huzuni mtangazaji nyota akijitia kitanzi

MARY WANGARI na MAUREEN ONGALA

HUZUNI umetanda katika kijiji cha Mkongani, eneo la Matsangoni, Kaunti ya Kilifi, baada ya mtangazaji wa zamani katika kituo cha redio cha Pwani FM, Sammy Ambari,48, kupatikana akiwa ameaga dunia nyumbani kwake.

Sammy almaarufu ‘Mtumishi’ alijitwalia umaarufu kupitia kipindi cha ‘Tumsifu Bwana’ kilichopeperushwa kila siku ya Jumapili kuanzia saa kumi na mbili asubuhi hadi saa tatu asubuhi, akisaidiwa na Ruth Masita kuendesha kipindi hicho.

Ndugu yake mdogo Morris Ambari amethibitisha kwamba ndugu yake huyo mkubwa aliaga dunia Jumapili.

“Nilimuita ndugu yangu kwa staftahi mnamo Jumapili akakataa na baadaye akapatikana amejitia kitanzi,” akasema Morris.

Alipatikana kwa chumba cha watoto kulala juu ghorofani katika nyumba yake.

Ndugu yake huyo mdogo amesema kwamba mnamo Agosti, Sammy alimdokezea kwamba alikuwa anapitia hali ngumu ya kifedha.

Hadi kufa kwake, Sammy amekuwa akifanya biashara na serikali ya Kaunti ya Kilifi kwa kusambaza bidhaa na huduma.

Ripoti ya upasuaji uliofanywa jana Jumatatu katika Hospitali ya Rufaa ya Kaunti ya Kilifi imethibitisha kwamba alijitia kitanzi.

Mwanahabari huyo alijitosa kwenye ulingo wa kisiasa baada ya kuondoka Pwani FM mwaka 2013.

Habari kuhusu kifo cha mwendazake ziliripotiwa kwanza Jumanne na Pwani FM kupitia ukurasa wake rasmi kwenye mitandao ya kijamii.

“Aliyekuwa mtangazaji wa kituo cha habari cha Pwani FM Sammy Ambari almaarufu kama Mtumishi ameaga dunia kwa kujitoa uhai nyumbani kwake eneo la Mkongani wadi ya Matsangoni kaunti ya Kilifi,” ilisema taarifa kutoka shirika hilo.

“Ambari alitangaza kipindi cha Tumsifu Bwana kila siku ya Jumapili kuanzia saa kumi na mbili jioni hadi saa tatu usiku.”

Inadaiwa kuwa kabla ya kujitia kitanzi, Mtumishi alikuwa akipambana na matatizo ya kiakili baada ya juhudi zake za kuwania katika chaguzi zilizopita kugonga mwamba.

Aidha, kisa hiki kimejiri huku kukiwa na hofu kutokana na kuongezeka pakubwa kwa visa vya watu kujitoa uhai nchini hali inayohusishwa na matatizo ya kimawazo hususan wakati huu wa gharama ya juu ya maisha.

“Kenya yafaa ipatie kipaumbele swala la afya ya akili,” alihoji Gilead Shuma.

Andrew Kipawa alisema, “Makiwa kwa familia, na marehemu apumzike kwa amani. Watu wanapitia wakati mgumu, ila wakuwashirikisha wanakosa.”

“Yatupasa tusipostahimili msongo wa mawazo tutafute huduma Kwa wataalamu wahusika Kwa mawaida kamilifu tusije tukawa wagonjwa wala kupoteza maisha kiholela,” alihoji Dominic Osoro.

Mashabiki na marafiki walimiminika kutuma risala za rambirambi kwa jamaa na familia ya marehemu huku wakimkumbuka kwa weledi wake alipokuwa mtangazaji.

“Tulishiriki kanisa moja miaka hio ya hapo nyuma. Waliimba pamoja na Emachichi zama hizo kwa kikundi Elim sounds,”aliomboleza Arthur Sipo.

“Namkumbuka sana huyu bingwa… asafiri salama… tutaonana baadaye na msemo wake wa ‘Je, Umekunywa Dawa?” alisema Harrison Ngowa.

Bakari naye alisema, “Waaahhh… tambua sana huyu mtumishi.”

“Namfahamu Sammy tukiwa naye pale Pwani FM kama Mtumishi wa Mungu, mpole na rafiki wa wengi. Mungu ailaze roho yake pahala pema,” alisema Tom Makinda.

Marehemu ameacha watoto watatu na mjane.

  • Tags

You can share this post!

Waathiriwa wa moto katika mtaa wa mabanda wa Mukuru-Hazina...

Wakurugenzi 7 wakanusha mashtaka ya kupora Sh1 bilioni za...

T L