NA MWANGI MUIRURI
BODI mpya ya wakurugenzi ya kampuni ya kununua na kuuza mashamba ya Embakasi Ranching, sasa inamtaka Naibu Rais Rigathi Gachagua kuisaidia kuzungumza na watu walioiba na kutumia ardhi ya wenye hisa.
“Changamoto kubwa tuliyo nayo ni kwamba wakurugenzi wa zamani waliwauzia walaghai sehemu ya ardhi, wakaongeza idadi ya wenye hisa na kuwagawia watu wengi vipande sawa vya ardhi. Walaghai hao walichukua nafasi hiyo na kuitumia ardhi ambayo si yao,” akasema mwenyekiti mpya wa kampuni hiyo, Bi Phideli Wangari.
Alisema kuwa “hiyo ndiyo hali waliyowekwa na mitandao ya wanyakuzi wa ardhi ambapo sasa tunaomba kuzungumza nao kuhusu vile tutarejeshewa mali tunayomiliki kihalali. Tunaomba walaghai hao watuhurumie”.
Alisema wahuni hao huenda mahakamani baada ya kunyakua ardhi, ambako huwa wanapata kibali cha kuitumia huku “wao wakibaki kama maskwota katika ardhi yao wenyewe, licha ya uwepo wa serikali”.
Bi Wangari alichaguliwa kuiongoza kampuni hiyo pamoja na wakurugenzi wengine wanane, kwenye mkutano wa kila mwaka uliokumbwa na mivutano, uliofanyika mjini Kiganjo, Kaunti ya Kiambu, Jumamosi wiki iliyopita.
“Kwa sasa, tunamtaka Bw Gachagua kufahamu kuwa umiliki wa kampuni hii uliwashirikisha wenyeji wa eneo la Mlima Kenya pekee. Hata hivyo, tunavyozungumza, tumepoteza umiliki mkubwa kutokana na ufisadi,” akasema.
Alisema kuwa kile wanachomhitaji Bw Gachagua kuwasaidia kwacho ni kuiwezesha kampuni hiyo kubuni utaratibu ambapo walaghai walionyakua ardhi ya wenye hisa wa halisi watawalipa ridhaa.
“Hatutaki kufuata njia ambapo makazi ya wale walionyakua ardhi yetu yatabomolewa. Wanaweza kuendelea kuimiliki ardhi hiyo, japo nao wawalipe fidia wamiliki halisi kulingana na bei iliyopo ya ardhi wakati huu,” akasema.
Kwenye mkutano huo, Mzee Michael Gitau, 85, alisema kuwa “Bw Gachagua anafanya kazi nzuri kupigania haki za mashamba ya wapiganiaji wa Mau Mau anayosema yalinyakuliwa na familia chache ambazo zimekuwa uongozini”.
Hata hivyo, Bw Gitau aliongeza kuwa Bw Gachagua “anasahau kuna mashamba ya Mau Mau yaliyonunuliwa kwa mpango wa vyama vya ushirika”.