• Nairobi
  • Last Updated February 25th, 2024 11:30 AM
Mashirika yapigania haki ya ‘boychild’ visa vya ulawiti vikiongezeka Kilifi

Mashirika yapigania haki ya ‘boychild’ visa vya ulawiti vikiongezeka Kilifi

NA MAUREEN ONGALA

KWA miaka mingi visa vya dhuluma za kijinsia kwa watoto wa kike vimekuwa vikiripotiwa katika Kaunti ya Kilifi, hali iliyochangia kwa visa ongezeko la idadi ya wasichana wadogo waliopata ujauzito.

Kupitia hatua mbalimbali, serikali ya kitaifa na ya kaunti pamoja na wadau na mashirika yasiyokuwa ya serakali waliungana pamoja na kuanzisha vita vikali dhidi ya dhuluma za kijinsia miongoni mwa watoto wa kike ikiweko kupiga marufuku disko matanga na sherehe za usiku ambazo zimekuwa chanzo kikuu cha mimba za mapema.

Sasa idara ya watoto katika kaunti hiyo imesema kuwa visa vya dhuluma za kijinsia zimechukua mkondo mwingine ambapo wavulana wengi wanalawitiwa.

Kulingana na afisa wa watoto eneobunge la Kilifi Kaskazini Bw Daniel Mbogo hali hiyo kwa njia moja au nyingine imechangiwa na ulegevu wa mashirika yasiyokuwa ya serikali wa kumtelekeza mtoto wa kiume na kumuacha.

Bw Mbogo anasema hali hii humfanya ‘boychild’ kuwa katika hatari ya kudhulumiwa, huku wakiendelea kumtetea na kumjenga mtoto wa kike.

Bw Mbogo aliwataka wadau kulichukulia swala hilo kwa uzito na kuingilia kati kwa haraka.

“Ninataka mashirika ambayo yanajihusisha pakubwa na mambo ya mtoto wa kike kuanza pia kumshughulikia mtoto wa kiume ambaye anaangamia kwa sasa,” akasema Bw Mbogo.

Hayo yanajiri huku kundi la kina mama la ‘Kilifi Mum’ katika Kaunti ya Kilifi, likizindiua kundi la kijamii la ‘Kilifi Boychild Empowerment’ kutetea haki za watoto wa kiume.

Akizungumza na Taifa Leo, mwenyekiti wa ‘Kilifi Mum’ Bi Kibibi Ali alisema kuwa mashirika mengi katika kaunti ya Kilifi wanatetea haki za  mtoto wa kike na wanawake.

“Tukianza na sisi Kilifi Mum, tumekuwa tukiweka zingatio katika kuwatetea watoto wa kike na wanawake wanapodhulimiwa na kwa sababu hiyo tumeona kuwa kuna changamoto kubwa mashinani kwani tumetenga mtoto wa kiume,” akasema Bi Ali.

Alisema kuwa ilikuwa ni makosa makubwa na ndipo kundi hilo likaamua kuchukua hatua ya kuweka mikakati ya kumkomboa mtoto wa kiume wa Kilifi.

“Siku hizi kuna mambo mengi machafu ambayo yanamlenga mtoto wa kiume na kwa sasa mtoto wa kike amekuwa na afueni kwa sababu anajua haki zake na anaweza kujitetea,” akasema.

Mwenyekiti wa kundi la kina mama la Kilifi Mum Bi Kibibi Ali akiongoza wadau wengine na vijana kukata keki wakati wa kuzindua shirika la Kilifi Boychild Empowerment CBO mjini Kilifi. PICHA | MAUREEN ONGALA

Alisema kuwa mbali na kuripotiwa visa vya watoto wa kike kunajisiwa, wanaendelea kupokea visa vya watoto wa kiume kulawitiwa na mwanamume mmoja au wanaume kadhaa.

Bi Ali alitoa mfano wa visa kadhaa vya ulawiti kikiwemo kisa kimoja ambacho mvulana alilawitiwa na babake.

Mwenyekiti wa kundi la kina mama la Kilifi Mum Bi Kibibi Ali akizungumza na wanahabari wakati wa kuzindua shirika la Kilifi Boychild Empowerment CBO mjini Kilifi. PICHA | MAUREEN ONGALA

Kisa kingine ni ambapo mvulana alivamiwa na kulawitiwa alipokuwa malishoni na pia mvulana mmoja alilawitia na genge la vijana watano.

Mwenyekiti wa Kilifi Boychild Empowerment CBO Bw Birya Menza alisema kikundi hicho kitakuwa sauti ya mtoto wa kiume.

“Kwa muda mrefu sasa mtoto wa kiume ametengwa na jamii na anayepatiwa kipaumbele ni mtoto wa kike huku akiendelea kupotea,” akasema.

Bw Birya alisema kuwa kasumba ya kuwa mtoto wa kiume hastahil kulalamika ama kulia anapopitia changamoto imemfanya kubaguliwa na jamii ilihali  yuko  na moyo ambao hauwezi kudhibiti changamoto nyingine.

“Mtoto wa kike akidhulumiwa   na mtoto wa kiueme inakuwa dhuluma ya jinsia lakini mtoto wa kike akimdhulumu mtoto wa kiume inachukuliwa kama swala la kawaida. Hakuna hatua inayochukuliwa ilia apate haki yake,” akasema.

Alitaka serikali na wadau kusimama imara na kumtetea mtoto wa kiume.

“Wanaume wengi wamepitia dhuluma za kijinsia kutoka kwa wanawake, wengine hata kupigwa, kuuawa na kunyimwa haki za ndoa kwa kuwa hawana mtetezi,” akasema.

Bw Birya alitoa changamoto pia kwa serikali ya kitaifa na ya kaunti na mashirika kwamba wanapoenda nyanjani kuwapelekea watoto wa kike sodo na mavazi ya ndani, wawakumbuke watoto wa kiume na kuwapelekea suruali za ndani.

“Wakati umefika wa kumkumbuka mtoto wa kiume na kumpa matumaini maishani kwa kumfanyia mambo ambayo atahisi kutobaguliwa,” akasema Bw Birya.

Ustadh Mahamoud Hambal kutoka shirika la Kenya Muslim Youth Alliance (KIMYA) alidai kuwa mtoto wa kiume ametengwa katika njia tofauti na jamii, mashirika na hata serikali ya kitaifa na ile ya kaunti.

“Katika tembeatembea yetu tulipata kuwa kdri mtoto wa kiume anavyoendelea kutengwa naye amezidi kujiachilia na anazidi kupotea,” akasema Ustadh Hambal.

Kiongozi huyo wa dini alisema kuwa imekuwa changamoto kuhusisha vijana wa kiume katika mipango tofauti kwani wengi wao walikata tamaa ya maisha na kujiona kuwa hawana umuhimu wowote katika jamii.

“Watoto wengi wa kiume wamekata tamaa na tunakuta ya kwamba inakuwa rahisi wao kushawishiwa kujiunga katika makundi haramu na uhalifu mkubwa kwa sababu wameona kwamba jamii, mashirika na serikali zote zimekosa kuwatambua na kutetea haki zao,” akasema.

Ustadh Hambal ambaye pia husimamia mpango ya kuwasaidia watoto maskini kwenda shule alisema kuwa mtoto wa kiume ametengwa hata katika upande wa elimu kwani mashirika mingi yanayosaidia watoto maskini kujiunga na Kidato cha Kwanza huwabagua.

Alitoa mfano na kusema kuwa kati ya nafasi 20 za watoto maskini wanaohitajika kujiunga na Kidato cha Kwanza, watoto wa kiume hupewa nafasi tano pekee.

“Ikiwa hali hii itaendelea kushuhudiwa, hatutakuwa na vijana wa kiume ambao wataenda shuleni. Hatutakuwa na vijana wa kusaidia taifa hili na itafikia wakati ambapo hata watoto wetu wa kike watakosa mabwana,” akasema.

Ustadh Hambal alisikitika kuwa watoto wengi wa kiume wanatumika kuuza dawa za kulevya na pia wao ni watumizi wakubwa wa mihadarati.

Kwa upande wake, mwalimu mkuu–rasi–wa shule ya upili ya wavulana ya Kilifi Township Bw Charo Katana alisema kuwa swala la mtoto wa kiume limekuwa nyeti kwa majira haya nchini kwani kiukweli wako hatarini.

“Idadi kubwa ya Wakenya ni vijana na haswa walio katika shule za msingi, za upili na vyuo vikuu na hicho ni kizazi kinachohitaji kusaidiwa kwa haraka sana kwani wanakumbana na changamoto nyingi maishani mwao,” akasema.

Alisema changomoto hizo huanzia kwa jamii na wanapofika shuleni, huwa wamebeba sehemu ya matatizo hayo na huyaendeleza, hali ambayo huwaathiri pakubwa.

“Changamoto hizi huwaathiri pakubwa wanapokuwa shuleni na kuwa pingamizi ya kufikia malengo yao ya maisha,” akasema.

Mwalimu Katana alisema kuwa swala la muhimu ni kuwa wavulana hao wanahitaji elimu ya kuwachanua akili zao wajitambue ya kwamba wana hadhi ya kujenga na hatima ya kuafikia na hayo yote yatakuja iwapo tu watapata watu wa kuwasaidia kuwapanua kimawazo.

Mwalimu Mkuu wa Shule ya Upili ya Wavulana ya Kilifi Township akizungumza na wanahabari wakati wa kuzindua shirika la Kilifi Boychild Empowerment CBO mjini Kilifi. PICHA | MAUREEN ONGALA

Alitoa changamoto kwa wazazi ambao aliwataja kuwa walimu wa kwanza wa watoto hao, kuchukua nafasi ya kutekeleza majukumu yao.

Alisema kuwa idadi kubwa ya wavulana wanaacha shule kufuatia changamoto za kinyumbani huku wazazi wa jinsia hiyo wakikosa kupatikana hata shuleni.

Mwalimu huyo mkuu aliwataja wazazi wa kiume kuwa wameachilia majukumu yao na kutwika majukumu ya kuwalea watoto wake zao ambao hata ndiyo huwapeleka na kuudhuria mikutano shuleni.

“Jukumu la mzazi si mavazi na chakula tu bali ushauri wa kila siku kwani usipomwongelesha mtoto wako, atapata mwingine ambaye atamuambia mambo tofauti ambayo yataathiri maisha yake,” akasema.

Kundi la Kilifi Mum ndilo liloanzisha mikakati ya kuunda Kilifi Boy Child Empowerment CBO ili kutetea mtoto wa kiume katika Kaunti ya Kilifi ambaye anaangamia kwa sasa.

  • Tags

You can share this post!

Wanachama wa UDA wanaokaidi Ruto kuadhibiwa

Watu sita waaga dunia Kikopey baada ya lori kupoteza...

T L