• Nairobi
  • Last Updated March 28th, 2024 11:42 PM
MCAs wa kiume Murang’a wamulikwa kwa kuwataka wenzao wa kike kwa lazima

MCAs wa kiume Murang’a wamulikwa kwa kuwataka wenzao wa kike kwa lazima

MWANGI MUIRURI Na MERCY KOSKEI

BAADHI ya viongozi wa kike Murang’a wameibua malalamishi kuhusu unyanyasaji wa kijinsia katika bunge la kaunti.

Wakiongozwa na Mbunge Mwakilishi wa Wanawake Betty Maina na Mbunge wa Maragua Mary wa Maua, wamedai wawakilishi wa wadi (MCAs) wa kike wanapitia dhuluma za kijinsia mikononi mwa wajumbe wenzao wa kiume.

Wakizungumza katika eneobunge la Kangema, wanasiasa hao walisikitika kuwa tabia hizo zimeanza kuathiri wenzao wa kike.

“Hii ni tabia mbaya sana. Tunazungumza kuhusu wanaume wakiwataka kimapenzi MCAs wa kike na wafanyikazi wengine wa kike katika bunge la kaunti. Mazuri aliyotupa Mungu yamekuwa shabaha,” Bi Wamaua alilalamika.

Kulingana mbunge huyo, kupenda na kuonyesha nia sio jambo baya ila wanafaa kufahamu kuwa ni chaguo la mtu binafsi kuamua ni nani atakayempenda.

Bi Maina alidai kuwa mara tu wanaume hao wanapokataliwa, wanashikwa na hasira na kuanza kuwaandama wanawake hao huku wakipinga kazi zao.

Alitishia kuwataja na kuwaaibisha wahusika wote katika bunge, ambao baada ya kukataliwa na baadhi ya wanawake, wanaanza kampeni za chuki na kuwazulia kashfa.

Akitoa onyo, mbunge huyo alisema kuwa hawatavumilia tabia za aina hiyo akielezea kwamba watapambana kama wanawake jasiri hadi itakapodhihirika kwamba hawako katika uongozi kugeuzwa roboti za ngono na wanaume waliopotoka kimaadili.

Hata hivyo, Spika wa bunge la kaunti hiyo Bw Johnson Mukuha na kiongozi wa wengi Bw Kibe Wasally walidinda kuzungumzia suala hilo.

Kulingana na mwakilishi mmoja, kumekuwa na mzozo kati ya wanawake na baadhi ya viongozi wakuu wa baraza kwa sababu ya masilahi mengi ambayo ni pamoja na idhini ya safari za nje na kujumuishwa katika kamati mbalimbali bunge la Kaunti ya Murang’a.

Alisema kuwa madai yaliyotolewa na Bi Maina na Wa Maua yanaweza kuchukuliwa tu kwa uzito ikiwa walalamishi watapiga ripoti kwa polisi au washukiwa wa njama hiyo kufichuliwa.

Hata hivyo, Bi Maina alisema: “Tunajua tunachosema na tunatahadharisha washukiwa hao kwamba hatutaitikia unyanyasaji wa kijinsia tukiwa tumelala chini, tutapigana na tutashinda.”

Naye Bi Wa Maua alisema: “Hakuna haja ya kutaka tuwataje wahalifu wakati wamekuwa wakitoa maoni ya ngono hadharani.”

  • Tags

You can share this post!

Wanagofu 110 kuwania taji la KCB East Africa Golf Tour...

‘Acheni domo mtupe mbinu mbadala za ukusanyaji ushuru’

T L