• Nairobi
  • Last Updated October 2nd, 2023 10:00 AM
Mke na mume wachimba shimo ndani ya ‘bedroom’ kuficha bangi

Mke na mume wachimba shimo ndani ya ‘bedroom’ kuficha bangi

NA RICHARD MUNGUTI

WASHTAKIWA wawili – mke na mumewe – waliochimba shimo ndani ya chumba chao cha kulala na kuficha bangi ya Sh63,930 wamepokezwa adhabu kali.

Mwanamke amefungwa mwaka mmoja akitumikia kifungo cha nje huku mumewe akipokezwa kifungo cha miaka miwili kavu gerezani.

Amina Abdi Kiyo na Francis Mwenda walipatikana na hatia ya kuchimba shimo ndani ya chumba cha kulala kusudi wafiche bangi kinyume cha sheria.

Mbali na kuficha kileo hicho ndani ya nyumba yao iliyo na vyumba vitano vya kulala, wawili hao walipatikana wakikuza mmea huo uliopigwa marufuku.

Mwenda hakufika kortini Ijumaa kwa vile alikuwa ameachiliwa kwa dhamana.

Hakimu mwandamizi mahakama ya Milimani Bernard Ochoi aliamuru Mwenda asakwe na kukamatwa kisha afikishwe kortini kuadhibiwa kwa makosa mengine mapya.

Kiongozi wa mashtaka James Gachoka aliomba mahakama itoe kibali cha kumtia nguvuni muuzaji bangi huyo.

“Hii mahakama imempata Francis Mwenda na hatia ya kuficha bangi ndani ya nyumba aliyokuwa akiishi na Amina Abdi Kiyo. Imemuhukumu kutumikia kifungo cha miaka miwili jela,” aliamuru Ochoi.

Hakimu pia alitoa kibali cha kumtia nguvuni mshtakiwa.

Akaamuru Bw Ochoi, “Naamuru polisi wamtafute na kumfikisha kortini Francis Mwenda atumikie kifungo kwa makosa ya kukuza ba kuficha bangi ndani ya chumba chake cha kulala. Ataanza kutumikia kifungo siku ile atakapokamatwa.”

Amina na mumewe Francis Mwenda walikabiliwa na shtaka la kuhifadhi mihadarati gramu 2,131 za bangi za thamani ya Sh63,930 mnamo Oktoba 17, 2019.

Walipatikana wakiwa na mihandarati hiyo katika eneo la Mwangaza, katika Kaunti ya Isiolo.

Amina Abdi Kiyo aliyeshtakiwa pamoja na mumewe Francis Mwenda aliagizwa awe akifanya kazi ya jamii katika Kaunti ya Isiolo.

Hakimu alimwagiza Amina afike katika kituo ch apolisi cha Kina ambapo afisa wa  urekebishaji tabia atamshauri kisha apewe kazi za kufanya.

Amina alihukumiwa kifungo cha nje baada ya kufichua bangi iliyokutwa na mfuko wa rangi ya zambarau ilikuwa ya mumewe.

“Mume wangu alinieleza ni bidhaa zake za kazi. Hakunieleza ni kazi gani,” Amina alimweleza hakimu akiomba msamaha.

  • Tags

You can share this post!

Alia warembo humkwepa wakidai hawakumbatii

Wanagofu 110 kuwania taji la KCB East Africa Golf Tour...

T L