NA LUCY MKANYIKA
WAKULIMA katika Kaunti ya Taita Taveta, wameelezea mahangaiko wanayopitia kwa vile ujenzi wa kiwanda cha ndizi ulikwama baada ya Sh110 milioni kutumiwa kwa mradi huo.
Kiwanda hicho kilichonuiwa kuongeza ubora kwa ndizi katika mpaka wa Taveta/Holili kilikuwa kimefadhiliwa na Muungano wa Ulaya (EU) kwa Sh110 milioni, na Serikali ya Kaunti ya Taita Taveta ilihitajika kuongezea Sh6 milioni.
Ujenzi ulikuwa umezinduliwa mwaka wa 2019, lakini kampuni ya Msuya Contractors Ltd iliyopewa kandarasi ilisitisha kazi mwaka 2022 ikidai Sh6 milioni.
Sasa mjengo uliopo na kiwanja chake vimegeuka makao ya wanyama kama vile panya, nyoka na mijusi.
Ndani ya jengo hilo, sakafu na sehemu za kuta zimeanza kubomoka huku kiwanja kikijaa nyasi na vichaka. Sehemu iliyonuiwa kuwa ya kupokea ndizi za wakulima, ishaharibika baada ya paa kung’olewa na upepo.
Bi Gladys Kingi, mmoja wa wakulima, alisema huwa wanapunjwa na madalali, hali ambayo imewafanya baadhi yao kuacha kilimo cha ndizi.
Afisa Mkuu wa Kilimo katika kaunti hiyo, Bw Steven Mcharo, alisema utawala mpya wa kaunti utahakikisha mradi huo umekamilishwa ndani ya mwaka mmoja ujao.
Alisema wanaendelea kutafuta washirika kufadhili ukarabati wa sehemu zilizoharibika, ujenzi wa sehemu nyingine zinazohitajika, na ununuzi wa mitambo ya kuongeza ubora kwa ndizi.