• Nairobi
  • Last Updated February 22nd, 2024 12:05 PM
Mung’aro aagiza daktari anayedaiwa kulewa kazini apelekwe hospitalini

Mung’aro aagiza daktari anayedaiwa kulewa kazini apelekwe hospitalini

NA ALEX KALAMA

GAVANA wa Kaunti ya Kilifi Gideon Mung’aro amemsimamisha kazi kwa muda afisa mkuu wa afya katika kituo cha afya cha Baolala kufuatia madai ya kuzembea kazi.

Gavana Mung’aro ameagiza afisa huyo kupewa likizo ya lazima ya miezi mitatu kabla ya hatima yake kujulikana.

Gavana huyo aidha ameamuru daktari huyo kufanyiwa matibabu katika muda huo wa likizo ya lazima.

“Nataka kutangaza yule daktari ambaye madai yameibuka kwamba amezembea kule Baolala apelekwe nyumbani kwa miezi mitatu na katika muda huo, mwanasheria wa kaunti, katibu wa kaunti na waziri wa afya mpelekeni katika hospitali akashughulikiwe. Nimeambiwa tatizo lake ni ulevi… si kwamba ana matatizo mengine… ni mlevi mpaka amekuwa mgonjwa,” akasema gavana huyo.

Hatua ya Munga’ro inajiri baada ya malalamishi ya diwani wa wadi ya Jilore Hamisi Jambo kuibua malalamiko kuhusu utepetevu wa afisa huyo wa afya katika kituo cha afya cha Baolala.

Diwani huyo aliibua madai ya kwamba alimuona daktari anayehudumu katika kituo hicho cha Baolala akiwa amelewa chakari wakati wa kazi.

“Nilienda pale na kamati ya afya ya bunge la kaunti na tukapata daktari pale akiwa ni mlevi,” alidai Bw Jambo.

Kwa upande wake waziri wa afya katika kaunti hiyo Peter Mwarogo amedokeza kuwa idara yake inalishughulikia suala hilo kwa mujibu wa sheria.

“Kabla ya kumfukuza mfanyakazi ni lazima tuwe tunafuata hatua za kisheria,” alisema Bw Mwarogo.

Aidha waziri huyo wa afya wa serikali ya Kilifi alikiri kuwa idara ya afya ya kaunti hiyo bado inakumbwa na changamoto nyingi ikiwemo uhaba wa madaktari.

“Bado tuko na matatizo ambayo yanakumba idara hii kwa sababu tuko na hospitali nyingi lakini madaktari ni kidogo. Kwa hivyo naomba mtupe muda ili tuweze kutatua shida hii,” alisema Bw Mwarogo.

  • Tags

You can share this post!

Amerika ilituambia tuwarudishe wakuu wa Worldcoin kwao,...

Mashirika ya kijamii yalalamikia ongezeko la visa vya...

T L