• Nairobi
  • Last Updated February 25th, 2024 11:30 AM
Naibu Gavana Kisii akabwa koo na ukoo wa Nyaribari akitakiwa kueleza ikiwa anaunga mkono Gavana Arati 

Naibu Gavana Kisii akabwa koo na ukoo wa Nyaribari akitakiwa kueleza ikiwa anaunga mkono Gavana Arati 

NA WYCLIFFE NYABERI

BAADHI ya viongozi na wazee kutoka ukoo wa Nyaribari sasa wanamtaka Naibu Gavana wa Kisii Dkt Robert Monda kuweka bayana ikiwa anamuunga mkono bosi wake, Gavana Simba Arati au la.

Viongozi hao kutoka Nyaribari ya Masaba na ile ya Chache, mnamo Jumatatu, Novemba 27, 2023 walionyesha hofu kwamba huenda Dkt Monda anapanga kuyoyomea serikalini na hawahusiki kwa vyovyote na uamuzi wake.

Haya yanajiri siku mbili tu baada ya Dkt Monda kuwakaribisha nyumbani kwake viongozi wa chama cha UDA Kisii, na wabunge wanaoegemea serikali ambao ni wakosoaji wakubwa wa Bw Arati.

Wakosoaji hao ni seneta wa Kisii Richard Onyonka, wabunge Silvanus Osoro (Mugirango Kusini), Daniel Manduku (Nyaribari Masaba), Japheth Nyakundi (Kitutu Chache Kaskazini), Mwakilishi wa kike Dorice Aburi na madiwani (MCAs) wengine.

Baada ya kuhudhuria hafla ya shukrani katika Kanisa Katoliki la Nyaburururu Jumamosi iliyopita pamoja na Spika wa bunge la Kitaifa Moses Wetang’ula, wabunge hao walifululiza moja kwa moja hadi kwa Bw Monda na kujikita kwenye kikao cha faragha ambapo walijadili siasa kwa zaidi ya saa matano.

Licha ya wabunge hao kudokeza baada ya kikao hicho cha faragha kwamba walijadili jinsi ya kuipeleka kaunti ya Kisii mbele, baadhi ya wandani wa Gavana Arati walidai kikao hicho kilikuwa cha kupanga njama ya kumhujumu Arati.

Hatua hiyo iliwakuta wakazi wengi wa Kisii kwa mshangao kwani tangu wautwae uongozi wa kaunti, wawili hao wamekuwa wakifanya kazi kwa ukaribu mno.

Wakihutubia wanahabari kuhusu yaliyojiri, wafuasi hao wa gavana walimtaka Dkt Monda ajitokeze na kutangaza msimamo wake, huku wengine wakimtaka ajiuzulu.

“Hatuhusiki kwa vyovyote na hatua ya Naibu Gavana kujiunga na wakosoaji wa Gavana Arati. Kama viongozi kutoka Nyaribari, hatukuhusishwa na hatua hiyo ni yake ya kibinafsi,” mmoja wa wazee hao aliyesoma taarifa ya pamoja alisema.

 Wazee hao walisema wanamuunga mkono kikamilifu Gavana Arati.

Walidokeza pia kuwa kiti alichonacho Dkt Monda ni cha Abanyaribari kutokana na makubaliano ya kugawa viti vya kaunti yaliyofanywa kabla ya uchaguzi mkuu wa 2022.

Hivyo, walidai si vyema kwa naibu gavana kujiamulia mwelekeo wake wa kisiasa.

  • Tags

You can share this post!

Simba jike atishia kuangusha Ripoti ya Kamati ya Maridhiano...

Uhispania Marathon: Cheptegei wa Uganda anyemelea rekodi ya...

T L