• Nairobi
  • Last Updated October 2nd, 2023 11:30 AM
Nakuru yapokea mitungi ya Oksijeni kuboresha huduma za afya

Nakuru yapokea mitungi ya Oksijeni kuboresha huduma za afya

NA MERCY KOSKEI

KAUNTI ya Nakuru imepokea mitungi 695 ya Oksijeni na vifaa vya usambazaji wa gesi hiyo kutoka kwa Amref Health Africa kupitia Wizara ya Afya ya serikali kuu.

Hatua hii inalenga kuhakikisha kuwa Huduma ya Afya ya Msingi (PHC) kwa wakazi wote kutoka maeneobunge 11 Nakuru imetekelezwa.

Kulingana na Waziri wa Afya wa kaunti, Jacqueline Osoro shehena hii inalenga kuongeza uhifadhi, usambazaji wa Oksijeni na matibabu katika vituo 12 vya afya kaunti nzima.

Akizungumza baada ya kupokea bidhaa hizo kutoka kwa Dkt Sospeter Gitonga mwakilishi Wizara ya Afya, Bi Osoro alisema kuwa vifaa hivyo vitatumika ipasavyo ili kuboresha utoaji wa huduma na kuhakikisha yeyote anayetembelea kituo cha afya atahudumiwa kwa wakati ufaao.

Alisema kuwa silinda tamba hizo za Oksijeni pia zitasaidia wagonjwa wanaosafirishwa kwa ambulensi hasa wanaohitaji kubadilishwa figo na pia kwa wale wanaohitaji huduma za kipekee.

Waziri wa Afya ya Kaunti ya Nakuru, Bi Jacqueline Osoro. Picha / Mercy Koskei

“Shehena ambayo tumepokea leo itawafaa sana wakazi wa Nakuru wanaohitaji matibabu ya Oksijeni, kutoka kwa watoto walio na nimonia hadi watu wazima walio na kifua kikuu na shida zingine za kupumua,” alisema Bi Osoro

Hospitali ya Rufaa ya Nakuru, itapokea usaidizi mkubwa kwani itapunguziwa rufaa.

Kwa sasa inatumia takriban lita 500,000 kila siku kutokana na idadi kubwa ya rufaa kutoka hospitali zingine za kaunti.

Bi Osoro alifichua kuwa mitungi hiyo itawekwa vitambulisho vya kipekee vya kaunti ya Nakuru na vituo vya afya vitakavyopokea ili kuzuia wizi wa mali ya umma.

Hafla hiyo ilihudhuriwa na Afisa Mkuu wa Huduma ya Afya Dkt John Murima, Msimamizi wa Matibabu wa Hospitali ya Rufaa na Mafunzo ya Kaunti ya Nakuru Dkt James Waweru pamoja na wawakilishi wa Amref.

Uwekezaji huu wa serikali ya kitaifa, Amref Health Africa na Global Fund unajumuisha utoaji wa mitambo 22 ya zalishaji wa Oksijeni, matangi 14 ya Oksijeni kwa ajili ya vituo vya ngazi vya juu, mabomba yote yakilenga uafikiaji wa Oksijeni na huduma bora kuokoa maisha.

Mpango huu unatarajiwa kunufaisha Wakenya ambao hapo awali walikuwa na tatizo la kupokea Oksijeni katika vituo mbalimbali vya afya kwa sababu ya uhaba wa mitungi ya gesi hiyo, kama ilivyoshuhudiwa wakati wa janga la Covid-19.

Waziri wa Afya ya Kaunti ya Nakuru Jacqueline Osoro akizungumza na Dkt Sospeter Gitonga kutoka Wizara ya Afya baada ya kupokea vifaa kuboresha huduma za afya Nakuru. Picha / Mercy Koskei
  • Tags

You can share this post!

Gaucho amlilia Uhuru Kenyatta amjengee nyumba

Seth Panyako ajiuzulu naibu mwenyekiti UDA akidai imefeli...

T L