• Nairobi
  • Last Updated February 29th, 2024 5:56 PM
Ndovu wakaidi Taita Taveta ‘wanaonyang’anya’ watu chakula

Ndovu wakaidi Taita Taveta ‘wanaonyang’anya’ watu chakula

NA LUCY MKANYIKA

WAKULIMA maeneo mbalimbali katika kaunti ya Taita Taveta wanalazimika kulala mashambani mwao ili kulinda mimea na mazao kufuatia kero ya ndovu wanaoongezeka kila uchao.

Wakulima hao wanasema visa vya ndovu kuvamia mashamba yao vimeongezeka, huku wakihofia kuwa huenda wakakosa chakula kutokana uvamizi wa wanyama hao.

Bw Renson Dio mkazi kijiji cha Jora alisema kuwa ndovu hao wamekuwa donda sugu linalosababisha wenyeji kuishi maisha ya ombaomba kwa sababu ya njaa na umaskini.

Kila siku, Bw Dio hutoka nyumbani kwake na kuelekea shambani ili kulinda mazao yake dhidi ya ndovu.

Alisema hana budi ila kulala shambani, kwani hawezi kupoteza mazao yake ambayo anategemea kumpa kipato na chakula kwa familia yake ya watoto wanane.

“Imebidi tuhame nyumbani na kuishi shambani kwa sababu msimu huu lazima tuvune,” akasema.

Katika shamba la ekari sita eneo la Jogholo, amepanda mahindi, maharagwe, njugu na kunde.

“Tumekuwa tukilima hapa kwa miaka mingi, lakini sijawahi kuona tatizo kubwa kama hili la mgogoro kati ya binadamu na wanyamapori. Ndovu wanakuja karibu kila usiku,’ alisema.

Wenyeji wanajaribu njia mbalimbali kufukuza ndovu ikiwa ni pamoja na kujenga ua kwa kutumia chupa za plastiki na kutumia manati kuwafurusha.

“Tumejaribu njia nyingi kuwafukuza, lakini siku hizi ni werevu na wenye nguvu sana,” akasema Bw Dio.

Aidha, amefuga mbwa wakali ambao wanabweka kumjulisha wakati ndovu wanapokaribia shambani.

Wakulima wengi Taita Taveta wanependekeza kuwepo kwa walinzi wa akiba kushughulikia tatizo la uvamizi wa wanyamapori.

Bw Harry Mwakai, mkazi wa kijiji cha Bungule, alisema walinzi wa akiba wanapaswa kuwa wenyeji ambao wanafunzwa na kupewa vifaa na shirika la wanyamapori, KWS, ili kusaidia katika usimamizi na usalama wa wanyamapori katika maeneo yao.

Alisema walinzi hao wataweza kusaidia na kujulisha KWS mapema ikiwa ndovu wamevamia.

“Walinzi wa KWS hawatoshi kusaidia kaunti nzima, na wanachelewa kushughulikia dharura. Wakati mwingine wao huwasili baada ya uharibifu kufanyika. Tunahitaji walinzi wa akiba kutoka jamii zetu ambao wanafahamu changamoto zetu,” alisema.

Mbunge wa Voi Bw Abdi Chome alisema anaunga mkono wazo hilo, akiamini kwamba askari wa akiba watasaidia kupunguza migogoro kati ya binadamu na wanyamapori na kuimarisha uhusiano mwema baina ya wanyamapori na wenyeji.

“Kama vile kitengo cha Walinzi wa Akiba wa Polisi (KPR) kiliundwa kusaidia polisi wa kawaida katika kudumisha usalama, ingekuwa muhimu kuunda kikosi kama hicho kusaidia KWS katika kuwafukuza wanyamapori kutoka maeneo ya jamii,” alisema.

Vilevile, mbunge wa Mwatate Bw Peter Shake aliahidi kushawishi serikali kuunda kikosi hicho na vilevile kuitaka serikali kuingilia kati na kupata suluhu ya kudumu kukabiliana na mgogoro kati ya binadamu na wanyamapori.

Kwa upande wake, afisa wa kaunti wa KWS Josephat Erupe alisema kuwa shirika hilo linajitahidi kukabiliana na wanyamapori wanaovamia makazi ya wenyeji.

Alidai kuwa shirika hilo linakabiliwa na ukosefu wa magari na maafisa wa kutosha kukabiliana na wanyamapori.

“Licha ya changamoto tunazopitia, tunaendelea kuweka mikakati ya kupunguza shida hii,” alisema.

 

  • Tags

You can share this post!

DJ Saint Kevin: Karen Nyamu anaelewa kupenda  

KEBS: Mafuta yaliyosemekana kuwa hatari ni salama

T L