• Nairobi
  • Last Updated April 18th, 2024 9:15 PM
Polisi wadaiwa kupalilia mbegu ya uhalifu jijini Nakuru

Polisi wadaiwa kupalilia mbegu ya uhalifu jijini Nakuru

NA MERCY KOSKEI

BAADHI ya maafisa wa polisi wanashukiwa kuwalinda wahalifu na hivyo kuchangia kuzuka upya kwa magenge ya wahalifu jijini Nakuru.

Kulingana na Kamishna wa Kaunti ya Nakuru Bw Loyford Kibaara, uchunguzi wake umebaini kuwa baadhi ya maafisa wa polisi katika maeneo ya Rhonda na Kaptembwa wamekuwa wakifanya kazi na magenge ya ugaidi.

Alisema hali hii inatatiza juhudi za kumaliza wahuni hao kwani maafisa huwapasha habari wanapotaka kufanya operesheni na kuingia mafichoni.

Kulingana na Bw Kibaara, baadhi ya maafisa wa ngazi za juu katika Idara ya Huduma za Polisi wameshindwa kukabiliana na magenge hayo kwa sababu wana ukuruba na wafuasi wa makundi hayo.

Bw Kibaara alisema kuwa hali hii ni chanzo cha kuibuka upya kwa magenge hayo hatari ambayo yamehusika katika visa vya uhalifu ambavyo vinajumuisha kudunga watu visu na wizi wa mabavu.

Alisema magenge hayo ambayo yamekithiri maeneo ya Pondamali, Sewage, Top ten, Stimaline, Jasho, Grogon na Posta yametia wakazi hofu, wengi wakiogopa kuendeleza biashara zao na shughuli nyingine za kawaida kwa utulivu.

Mtaa wa Stimaline jijini Nakuru. Mtaa huu ni miongoni mwa mitaa katika jiji hilo ambayo inakumbwa na visa vya uhalifu. PICHA | BONIFACE MWANGI

Kwa sasa waakazi wa Rhonda na Kaptembwa wanaishi kwa hofu kutokana na hali hii, wengi wakiomba polisi kushika doria.

Bw Peter Okoth, mkazi wa Kaptembwa ambaye alipoteza mwanawe Kennedy Omondi wiki tatu zilizopita, alisema kuwa kijana huyo aliacha familia changa–mke na mtoto wa umri wa mwaka mmoja na nusu.

Kulingana na Bw Okoth, Omondi aliondoka na rafiki yake kuenda kununua miraa katika kituo cha kibiashara na magari mawili yakapita kabla ya pikipiki iliyokuwa na wahalifu kutokea.

Alisema watu hao waliwazidi nguvu na kumuua Omondi papo hapo na kumwacha rafiki yake akiwa na majeraha mabaya. Alikimbizwa katika hospitali  ya rufaa ya Nakuru na wasamaria wema ili apate matibabu.

Bw Okoth alisema marehemu kijana wake aliyekuwa na umri wa miaka 29 alifanya kazi katika maeneo ya ujenzi na alikuwa mlezi ambaye alihakikisha kwamba wazazi wake na ndugu zake walitunzwa vyema.

Mkazi mmoja ambaye hakutaka jina lake litajwe alisema kuwa, magenge hayo hutumia mapanga, vyuma, na shoka.

Alisema genge hilo la kihuni limekita kambi maeneo ya Kaptembwa na Rhonda na bado wahalifu hao wanaendelea kusajili wanachama wengi zaidi.

Mkazi huyo alibaini kuwa kundi la Mauki limekuwa likizunguka na pikipiki zinazobeba watu wanne wakiwashambulia watu kwa visu na kuwaitisha fedha.

“Tunaishi kwa hofu; wanazunguka tu wakidunga watu visu na kunyanyasa yeyote njiani. Waliapa kwamba watalipiza kisasi kifo cha kiongozi wao. Hofu yetu ni kwamba maisha ya watu wasio na hatia yatapotea,” alisema.

Hata hivyo, Kamishna alitangaza mipango ya kuifanyia marekebisho kamati ya Nyumba Kumi, akidai kuwa timu iliyopo sasa haijafanya kazi.

Kulingana naye, kamati ya sasa imetishwa na haiko katika uwezo wa kutekeleza majukumu yao ipasavyo.

Bw Kibaara alibainisha kuwa msako mkali uliofanywa katika maeneo ya Bahati, Nakuru Mashariki na Nakuru Magharibi umezaa matunda ambapo washukiwa 380 walikamatwa.

Washukiwa hao wanasemekana kuwa wanachama wa magenge matano ikiwa ni pamoja na Mauki, Watized na Confirm. Vikundi hivyo vinafanya kazi kutoka mashambani huko Rhonda na Kaptembwa.

Bw Kibaara alisema makundi hayo yamekuwa yakijihusisha na mashambulio ya kulipiza kisasi, jambo ambalo limesababisha vifo vya baadhi ya wanachama hao, makabiliano ambayo yamewatia wananchi wasiwasi.

Kwa vijana zaidi ya 350 wanaoshukiwa kuwa wanachama wa magenge mbalimbali ya uhalifu wametiwa mbaroni.

Katika operesheni iliyoendeshwa Jumatatu usiku, kiongozi wa genge la Mauki aliyetambulika kwa jina la Solomon Mburu ni miongoni kwa vijana waliotiwa mbaroni.

Kukamatwa kwao kunajiri siku moja baada ya kikosi cha usalama cha kaunti hii kutangaza operesheni ya kali ili kuwaondoa magenge ya wahalifu katika maeneo bunge ya Nakuru Mashariki na Magharibi.

Maafisa hao pia walinasa silaha zinazoshukiwa kutumiwa na magenge hayo kuwashambulia watu.

Akizungumza wakati wa kikao na wanahabari Jumanne, Juni 7,2023 katika kituo cha Polisi cha Kaptembwa, Kamishna Kibaara alisema kuwa kwa muda wa mwezi mmoja kumekuwa na ongezeko la magenge haramu.

Kulingana na Bw Kibaara makundi ya Confirm, Watizedi na Mauki yamezidisha vitendo vyao vya uhalifu katika maeneo mbalimbali ya Nakuru huku mashambulio ya hivi majuzi yakiwa ni ya kulipiza kisasi miongoni mwao.

“Tunafanya hivi kwa sababu wengine wanaweza kudhani tunawakamata vijana ambao tunapaswa kuwasaidia lakini hawa ni wahalifu. Aina ya silaha wanazomiliki ni hatari. Kiongozi wao alipatikana na silaha,” alisema

Mnamo Juni 2022, aliyekuwa Waziri wa Usalama wa Ndani Dkt Fred Matiang’i alimteua Peter Mwanzo kama mkuu wa polisi wa Kaunti ya Nakuru baada ya visa vya uhalifu kuongezeka katika eneo hilo.

Bw Mwanzo alichukua nafasi ya Bi Beatrice Kiraguri wakati ambapo magenge yaliyopangwa yalikuwa yakihangaisha na kuwaua watu katika kaunti za Rift Valley.

Wakati wa uongozi wake, Bw Mwanzo aligonga vichwa vya habari alipokuwa akikabiliana na magenge hayo huku ripoti zikisema kiwango cha uhalifu kilipungua.

Mnamo Julai 2022, aliongoza operesheni iliyosababisha kukamatwa kwa wahalifu sita waliowaua wanawake katika eneo la Mawanga.

Genge lilikuwa likiongozwa na Evans Kebwaro ambaye alihojiwa na maafisa wa upelelezi kutoka Idara ya Upelelezi wa Jinai (DCI) akawataja Julius Otieno, Josephat Simiyu, Dennis Mmbolo, Isaac Kinyanjui na Makhoha Wanjala kuwa wanachama wa genge lake.

Miongoni mwa watu wasio na hatia waliopoteza maisha katika mauaji hayo ya kutisha ni pamoja na Grace Wanjiru,20, Susan Wambui,38, Diana Opicho,23, Beatrice Akinyi,21, Judy Nyambura,40, Shadiah Cheupe,17, na Rimsy Wanjiru,11, ambao waliuawa katika tarehe tofauti kati ya Juni na Julai 2022.

  • Tags

You can share this post!

Ushuru: Wabunge waonya Ruto

Naibu Rais: Nimeokoka na majina yangu kamili ni Geoffrey...

T L