• Nairobi
  • Last Updated December 8th, 2023 10:25 PM
Polisi wasaka mshukiwa anayetembea akiwa amejihami kwa shoka

Polisi wasaka mshukiwa anayetembea akiwa amejihami kwa shoka

NA MWANGI MUIRURI

POLISI Murang’a wanamsaka mshukiwa wa wizi wa mabavu ambaye inadaiwa kuwakumbatia, kuwapapasa na kuwabusu waathiriwa wake akiwapora huku akiwa amejihami kwa shoka.

Wenyeji wamempa mshukiwa huyo jina la majazi la ‘Wagathanwa Muhambati’ yaani ‘Wa shoka mpapasaji’.

Aidha, inadaiwa mwanamume huyo huvamia maboma ya watu na kuanzia na kuvunja dirisha ambapo anamwaga petroli kwa nyumba.

“Akishamwaga petroli hiyo, anakuambia upitishie yeye pesa na simu kwa dirisha la sivyo arushe moto ndani ya hiyo nyumba,” akasema mmoja wa waathiriwa, Wakili Mwangi Kamau.

Naye Bi Sarah Wangui, 48, ambaye ni mchuuzi katika soko la Mbombo, anadai kuwa alikutana na mshukiwa huyo mnamo Agosti 12, 2023, katika barabara ya kutoka Mbombo kuenda Kamuiru mwendo wa saa tano usiku.

“Ni mwanamume mnene na mwenye uso wa bapa. Aliweka shoka lake kwa kichwa changu na haja ndogo ikanitoka bila ya kujielewa. Aliniuliza ikiwa nilikuwa tayari kushirikiana naye na nikasalimu amri na ndipo akaweka shoka lake ndani ya kabuti alilokuwa amevaa,” akasema Bi Wangui.

Bi Wangui anasema mshukiwa huyo alimpapasa bila hiari yake lakini “furaha yangu ni kwamba hakunibaka”.

Ingawa hivyo, alipojitoma kwa shamba la mahindi lililokuwa karibu, aliniacha hapo barabarani nikiwa sina pesa, simu na hata kikapu changu cha bidhaa za sokoni,” asema.

Naye Joseph Kyende ambaye ni kibarua kwa shamba moja eneo hilo, anasema alikuwa akitembea kurejea nyumbani kutoka kwa baa moja eneo la Kandundu.

“Nilijipata nimekumbatiwa na mwanamume mzito kwa uzani. Alianza kunipapasa na kimoyomoyo nikajiambia siku yangu ya kwanza kulawitiwa ilikuwa imefika. Nilianza kupambana na ndipo aliweka shoka kwa shingo yangu. Nilisikia sauti kwa kichwa changu ikiniuliza kati ya kulawitiwa na kuchinjwa kwa shoka ni gani afadhali,” asema.

Kabla ya ajijibu, mwanamume huyo alitoweka na ndipo aligundua kuwa alikuwa ameporwa katika kisa hicho cha saa tatu na nusu usiku.

Ripoti za waathiriwa zinazidi kupigwa katika vituo vya polisi vya Kambirwa, Mbombo na Murang’a.

Wanaelezea kwamba wamepitia hayo ndani ya kipindi cha wiki tatu zilizopita.

Mshukiwa bado hajanaswa. Anasemekana kuvamia maeneo ya Kandundu, Samar, Kamuiro, Gutungano, Mbombo, Kambirwa na Muthigiriri ambako baadhi ya matajiri walio na makao mbadala wamehama kutokana na taharuki iliyotanda eneo hilo.

Inakisiwa kuwa zaidi ya watu 30 wamejipata katika uvamizi wa mhalifu huyo.

Chifu wa Township Bw Charles Muna, baada ya kufikiwa na wenyeji waliomsihi awasaidie kumnasa mshukiwa huyo, amesambaza picha za mshukiwa huyo mitandaoni, akiwataka wenyeji washirikiane na serikali ili kumnasa.

“Inadaiwa kwamba alihamia eneo hili kutoka Kaunti ya Kiambu alikokuwa anatumia mbinu hiyo kuwatesa wakazi,” akasema.

Kinachokera wenyeji ni kwamba Mkuu wa Idara ya Upelelezi wa Makosa ya Jinai (DCI) Kaunti ya Murang’a Bi Cecilia Mugambi hajatoa taarifa yoyote kuhusu taharuki hii.

“Hata kamanda wa polisi wa Murang’a Bw Mathiu Kainga na Kamishna Patrick Mukuria hawajatutembelea kutufariji. Huyu jambazi ametuwekea kafyu kwa kuwa ili kumhepa ni lazima tutembee kabla ya giza kuingia,” asema Bw Stephen Warui wa Kijiji cha Mumbi.

  • Tags

You can share this post!

Serikali yagundua ruzuku kwa mafuta inafaa

CHARLES WASONGA: Wengi kutoka familia maskini watakosa...

T L