• Nairobi
  • Last Updated November 28th, 2023 6:30 PM
Rais Ruto ‘kuvamia’ tena ngome ya Raila kusaka umaarufu kupitia uzinduzi wa miradi ya maendeleo

Rais Ruto ‘kuvamia’ tena ngome ya Raila kusaka umaarufu kupitia uzinduzi wa miradi ya maendeleo

NA GEORGE ODIWUOR

RAIS William Ruto anatarajiwa kurejea Luo Nyanza kuanzia Ijumaa hii kuzindua miradi mbalimbali ya maendeleo.

Ziara hiyo imefasiriwa kama sehemu ya mikakati yake ya kuimarisha umaarufu wake katika eneo hilo ambalo ni ngome ya kisiasa ya Kinara wa Upinzani Raila Odinga.

Rais Ruto ataanza ziara yake Kaunti ya Homa Bay kisha Kisumu ambako anatarajiwa kuandamana na viongozi wa Azimio na wale wa Kenya Kwanza kufungua miradi ya maendeleo.

Atakuwa akizuru Homa Bay kwa mara ya nne tangu ashinde uchaguzi mkuu uliopita.

Siku chache baada ya kuapishwa, Rais Ruto alizuru Homa Bay ila ziara hiyo ilisusiwa na wabunge wa ODM kutoka kaunti hiyo, Gavana Gladys Wanga na Seneta Moses Kajwang’.

Ziara nyingine mbili alizofanya zilichangamkiwa na upinzani pamoja na viongozi wa ODM.

Jana Jumamosi, Septemba 30, 2023, Bi Wanga, Waziri wa Teknolojia na Mawasiliano Eliud Owalo na Katibu katika Wizara ya Usalama wa Ndani Raymond Omollo walizuru mradi wa ujenzi wa bandari ambao unatarajiwa kufunguliwa na Rais na itaimarisha uchukuzi majini.

Bandari zingine zitajengwa katika maeneo yanayopakana na Ziwa Viktoria kwenye Kaunti za Homa Bay, Kisumu na Siaya.

Wanasiasa hao waliandamana na Mwenyekiti wa Mamlaka ya Bandari Nchini, William Ruto ambaye miradi itakayozinduliwa itakuwa chini ya uangalizi wake.

Alisema miradi yote itagharimu Sh1.5 bilioni na pia serikali itanunua meli kwa kima cha Sh600 milioni kutumika katika usafiri Ziwa Viktoria.

Kufuatia ziara hiyo, Bi Wanga alisisitiza kuwa kujumuika kwake na Rais Ruto hakufai kufasiriwa kuwa amegura chama cha ODM.

“Katiba inatoa ruhusa kwa serikali ya kaunti na ile ya kitaifa kushirikiana kuwahudumia raia. Uhusiano wetu utakuwa kwa msingi wa maendeleo ila kisiasa nipo ODM na uaminifu wangu ni kwa chama hicho,” akasema Bi Wanga.

Bw Omollo naye aliwataka wakazi wa Nyanza wamkaribishe Rais na akawaomba wakome kuharibu mali ya umma hasa wakati wanapoandaa maandamano.

“Katiba inawaruhusu kuandamana ila lazima mfanye hivyo kwa amani bila kuharibu mali ya umma,” akasema Bw Omollo.

 

 

 

  • Tags

You can share this post!

Mtoto Jasmine Njoki azikwa mshukiwa mkuu wa mauaji...

Ugumu wa maisha wasukuma wanafunzi wa vyuo kuishi kama mume...

T L