• Nairobi
  • Last Updated February 22nd, 2024 2:11 PM
Seneta Nyutu: Mabawabu wa Del Monte huenda wametekeleza mauaji kama ya Shakahola

Seneta Nyutu: Mabawabu wa Del Monte huenda wametekeleza mauaji kama ya Shakahola

NA MWANGI MUIRURI
SENETA wa Murang’a Bw Joe Nyutu sasa anamtaka Rais William Ruto kutoa amri kikao cha majirani wa shamba la kizungu la Del Monte lililoko kaunti hiyo kiandaliwe kupata ukweli kuhusu ukiukaji wa haki za kibinadamu.

Alisema kwamba huenda mabawabu wa shamba hilo wawe wametekeleza janga lingine sawa na lile la mauaji ya Shakahola, akisema kwamba bwawa kubwa la kampuni hiyo linapaswa kufunguliwa maji kubaini ikiwa kuna mabaki ya waliopotea.

Kampuni hiyo ya Kimarekani hukuza mananasi katika shamba la ekari 32, 000, na kando na kuyauza nje ya nchi huwa inaunda juisi maarufu ya Del Monte.

Bw Nyutu anashikilia kuwa kuna vijana wengi ambao wametoweka na mara ya mwisho kuonekana walikuwa mikononi mwa mabawabu hao.

“Mabawabu hao hudai kuwa mananasi yake huwa yanaibwa na baadhi ya vijana majirani. Katika misako ya kuwapata washukiwa, ndipo kila aina ya kilio huzuka ambapo vijana wengi huachwa na majeraha mabaya ya kupigwa na kulishwa majibwa huku wengine wakitoweka milele,” akasema Bw Nyutu.

Seneta Nyutu alisema kuwa kuna baadhi ya wadau ambao hukaa kimya msururu wa matukio hayo yakifanyika kwa msingi kwamba kampuni hiyo huajiri watu, hulipa ushuru na ni ya taifa rafiki wa Kenya.

“Hatutakubali ukoloni mamboleo kwa msingi wowote ule. Hili ni taifa la utaratibu wa kisheria na ni lazima mkondo wa haki ufuatwe. Ukiibiwa hapa nchini huna ruhusa ya kutekeleza kisasi cha kuua na kulemaza,” Bw Nyutu akasema akiwa Kaunti Ndogo ya Kandara.

Nyutu aliongeza kwamba “huku tukifanya juu chini kuunda nafasi za kazi ili tuwahami vijana wetu na riziki, hatutakubali umaskini wetu kuadhibiwa kupitia mauaji sawa na yaliyotekelezewa mababu zetu na wakoloni”.

Seneta Nyutu alisema kwamba “huwezi ukaja hapa kwetu Murang’a kutoka Amerika, upate mgao wa shamba letu huku wengi wetu wakiwa hawana hata kwa kuzikwa, uwe katika biashara ya mabilioni ukitumia urithi na jasho letu kisha ahsante yako iwe ni kutuua na kutugeuza kuwa viwete”.

Kupitia taarifa rasmi, kampuni hiyo ya Del Monte kupitia Mkurugenzi wake mkuu, Bw Stergios Gkaliamoutsas ilisema kwamba kampuni hiyo iko tayari kuungana na vitengo vya uchunguzi kupata ukweli wa suala hilo.

“Haki za kibinadamu ni mojawapo ya sera dhabiti katika nembo yetu. Tuko tayari kushirikiana na vitengo vyote husika kuweka suala hili uwazi.”

[email protected]

 

  • Tags

You can share this post!

Tanzia: Olesia wa Kenya Lionesses aaga dunia

Barabara za lami mpya zafanya Industrial Area kung’aa

T L