• Nairobi
  • Last Updated April 18th, 2024 9:15 PM
Serikali ya kaunti kutuza watunza mazingira

Serikali ya kaunti kutuza watunza mazingira

NA KALUME KAZUNGU

SERIKALI ya Kaunti ya Lamu, imetangaza mpango wa kuwazawadi watunzaji mikoko na wapanzi wa miti eneo hilo kama njia mojawapo ya kuwatia moyo.

Gavana wa Lamu, Issa Timamy anasema ili kutimiza malengo ya kaunti ya kupanda miti milioni moja na pia nchi kupanda miti bilioni 15 kufikia 2032, ni vyema kila eneo nchini kuibuka na mbinu zitakazopiga jeki mpango huo.

Juma lililopita, serikali ya kaunti ya Lamu kupitia kwa gavana Timamy ilitangaza kutenga Sh1 milioni kwa minajili ya kusaidia shughuli za kupanda miti eneo hilo.

“Kama kaunti, tumeafikia kutambua kila kundi linaloendeleza shughuli za utunzi wa mazingira, ikiwemo kupanda miti eneo hili. Tayari nimeagiza kuwe na mpango ambapo kila kundi litawasilisha ripoti kuhusu ni miti mingapi imepandwa, wapi na inaendelezwa vipi kabla ya kutuzwa fedha. Tukifanya hivyo ninaamini hilo lengo la kupanda miti bilioni 15 nchini kufikia 20312 litatimia,” akasema Bw Timamy.

Naibu Kamishna wa Kaunti ya Lamu, Bw Charles Kitheka aliwasifu wakazi wa Lamu kwa juhudi zao katika kupanda na kutunza miti, hasa mikoko.

Kwa mujibu wa rekodi kutoka kwa Shirika la Huduma za Misitu nchini (KFS), Lamu iko na asilimia karibu 65 ya msitu wa mikoko, ikilinganishwa na maeneo mengine ya nchi.

“Ninawashukuru wananchi wa hapa kwa kujitolea kutunza misitu. Ninaamini tukishikana tutafaulisha nyongeza ya asilimia 30 ya misitu kpote nchini kufikia mwaka 2032. Tujiepushe na uharibifu wa misitu,” akasema Bw Kitheka.

 

  • Tags

You can share this post!

Harusi ya kukata na shoka ya wanandoa wenye ulemavu kuskia...

Polisi wapata viungo zaidi vya mwanamume

T L