• Nairobi
  • Last Updated February 25th, 2024 9:50 AM
Shule ya Moi Kabarak Nakuru yaendelea kuficha matokeo yake ya KCPE 2023

Shule ya Moi Kabarak Nakuru yaendelea kuficha matokeo yake ya KCPE 2023

NA MERCY KOSKEI

SHULE ya msingi ya kibinafsi ya Moi Kabarak katika Kaunti ya Nakuru, imesalia kimya kuhusu matokeo yao ya Mtihani wa Kitaifa Darasa la Nane (KCPE) 2023 yaliyotolewa mwishoni mwa juma.

Shule hiyo huwa ya kwanza kuweka wazi matokeo yao, lakini siku ya Alhamisi, Novemba 23, 2023 Waziri wa Elimu Ezekiel Machogu alipotoa rasmi matokeo, haikufuata mkondo wake wa zamani.

Wanahabari walipozuru shule hiyo, usimamizi ulikwepa kuzungumza.

Siku ya matokeo kutangazwa, mazingira ya shule hiyo yalikuwa na shughuli haba.

Jambo hilo lilionekana kuwa kinyume na tikadi zake, ambapo wanafunzi, walimu na wazazi hukusanyika kusherehekea matokeo bora na kisha kuhutubia wanahabari.

Kwa sasa shule hiyo imekata rufaa kwa Baraza la Mitihani Nchini (KNEC) kuhakiki matokeo iliyopata, ikilalamikia kutopewa alama halali.

Mwalimu Mkuu Kiptoo Nelson, katika taarifa mnamo Ijumaa, Novemba 24, 2023 alisema kama shule hawajaridhishwa na matokeo hayo kwani hayaakisi uwezo wa wengi wa wanafunzi wake.

“Tulipokea matokeo ya KCPE ya 2023 baada ya matangazo kutoka kwa Katibu wa Baraza la Mawaziri, Wizara ya Elimu lakini kama shule, hatujaridhishwa na matokeo. Kwa hivyo, tumetoa wito kwa KNEC kufanya mapitio na tunatumai kwamba itashughulikia suala letu na kuchukua hatua za dharura,” akabainisha mwalimu huyo.

Mwaka jana, 2022, shule hiyo iliibuka kuwa miongoni mwa shule bora nchini huku mmoja wa wanafunzi wake akizoa alama 425.

Mtahiniwa huyo aliorodheshwa kati ya 10 bora ngazi ya kitaifa.

Shule hiyo ilikuwa na watahiniwa 246 na zaidi ya watahiniwa 80 waliopata alama zaidi ya 400.

Aidha, wastani wa alama 385.43.

Katika KCPE 2023, shule zimeibua malalamishi kuhusu ujumuishaji wa matokeo, baadhi ya alama zikiibua maswali chungu nzima.

KNEC, hata hivyo, imekiri kuwepo kwa dosari kwenye baadhi ya matokeo.

 

  • Tags

You can share this post!

Ruto asema serikali itaanza kukopa mama mboga na wahudumu...

Wakulima wageukia kufuga nyuki kutimua wezi wa mazao...

T L