NA MWANGI MUIRURI
POLISI katika Kaunti ya Murang’a wamemkamata mwanafunzi wa Chuo Kikuu cha Nairobi (UoN) mwenye umri wa miaka 21 aliyefumaniwa peupe Jumamosi jioni, Septemba 16, 2023 akimnajisi dada yake mwenye umri wa miaka 10.
Mkuu wa Polisi eneo la Kigumo, Kiprono Tanui, alisema kisa hicho kilitokea katika kijiji cha Mariira.
“Ni kweli mwanamume huyo yuko kizuizini na anatusaidia na uchunguzi. Majirani waliwadokezea polisi kuhusu kisa hicho ambapo OCS wetu aliwaongoza maafisa kuvunja mlango na kumkuta akiwa uchi kitandani na dada yake,” alisema.
Bw Tanui alisema msichana huyo alipelekwa katika Hospitali ya Kigumo kufanyiwa uchunguzi wa kimatibabu na kubaini kuwepo tendo la ngono.
“Hali ya kushuhudia tendo hilo ilitupa msingi thabiti wa kumkamata mwanamme huyo. Tunasubiri sasa ripoti kamili ya kimatibabu ambayo pia itajumuisha uchunguzi wa chembechembe kutuwezesha kukusanya ushahidi wa kutosha,” alisema.
Taarifa ya polisi ilisema mshukiwa alipatikana kitandani pamoja na msichana aliyeonekana kupumbazwa kwa dawa akiwa amelala kando yake uchi vilevile.
“Kulikuwa na dalili kuwa msichana huyo alikuwa amenajisiwa kwa sababu alikuwa analia na alionekana mnyonge. Alipelekwa hospitalini kufanyiwa vipimo vya kimatibabu. Ripoti itawasilishwa,” ilisema taarifa.
Seneta wa Kaunti ya Murang’a, Bw Joe Nyutu aliwahimiza wakazi eneo hilo kushirikiana na polisi kupiga vita kusambaa kwa matumizi ya mihadarati.
“Tunajiaibisha mno. Visa hivi ni doa kwa fahari na hadhi yetu. Kushuka hadi viwango duni kiasi hicho vya kupotoka kimaadili ambapo hatuna urazini tena kunasikitisha mno,” alisema.