• Nairobi
  • Last Updated February 22nd, 2024 12:05 PM
Upekee wa punda wa Lamu katika uchukuzi na usafirishaji bidhaa

Upekee wa punda wa Lamu katika uchukuzi na usafirishaji bidhaa

NA KALUME KAZUNGU

UKIDHANIA mizigo mizito hubebwa au kuburutwa kwa kutumia kreni, tingatinga, magari au mashine nyingine maalum pekee kutoka sehemu moja hadi nyingine, katika kisiwa cha Lamu mambo ni tofauti.

Hapa utapata punda wengi wakitumiwa na wakazi kusafirisha au kuburuta mizigo mizito, ima iwe ni vyuma vya kujengea, mawe, mbao, simiti, na mchanga kutoka mtaa mmoja hadi mwingine.

Kinyume na sehemu nyingine za nchi ambapo punda hutundikwa mikokoteni wanaposafirisha mizigo au shehena, ni Lamu pekee ambapo punda hupandwa, kuparamiwa, kubandikwa mizigo au shehena husika, iwe ni mizito au hafifu kwenye migongo yao moja kwa moja.

Punda wa Lamu (kulia) akiwa amebeba mizigo moja kwa moja kwenye migongo yao. Punda wa Lamu ni wa kipekee katika utoaji wa huduma za uchukuzi na usafirishaji wa mizigo. PICHA | KALUME KAZUNGU

Upitapo katikati ya vishoroba vya mji wa kale wa Lamu au mbele ya kisiwa hicho, si jambo geni kupishana na punda wakiwa wamebebeshwa mizigo hiyo migongoni, wakitia juhudi kuiburuta, ilmradi ifike eneo inakolengwa kushukishwa.

Ni kisiwani Lamu ambapo punda wana uzoefu mkubwa katika kubeba mizigo, hasa mizito bila utata wowote.

Hali hiyo ni kinyume kwa punda wa sehemu zingine nchini ambao huzua purukushani na kurusha mateke na makeke na hata kujeruhi wanaowatumisha kudhihirisha wazi kwamba katu hawapendezewi na jukumu la kubebeshwa mizigo.

Mwanamume akiwa amebebwa kwa punda. PICHA | KALUME KAZUNGU

 

Mwenyekiti wa Muungano wa Wamiliki wa Punda kisiwani Lamu, Bw Omar Kidege anasema punda ni msaada mkubwa kwa eneo hilo, akitaja kuwa iwapo mnyama huyo hangekuwepo, basi miji ya Lamu kama vile ule wa kale wa Lamu, Shela, Matondoni, Kipungani, Kizingitini, Pate, Siyu, Faza na mingineyo haingekuwepo katika dunia ya leo.

Lamu iko na idadi ya punda wapatao 10,000.

Ikumbukwe kuwa baadhi ya miji kama vile ule wa kale wa Lamu haitumii magari au baiskeli, hatua ambayo ni harakati za kuhifadhi historia, hadhi na ukale wa miji hiyo.

Vyombo vya pekee vitumiwavyo hapa ni mikokoteni na punda kusafirisha abiria na mizigo au watu kutembea kwa miguu.

Bw Kidege anafafanua kuwa ni punda waliojenga nyumba zote zipatikanazo Lamu.

“Sisi hutumia punda kubeba mawe, vyuma vya kujengea, simiti, mchanga, mbao, mabati, makuti, misumari na kila kitu. Hii ina maanisha kuwa hizi nyumba uzionazo kwenye miji ya Lamu leo hii zimejengwa kupitia mchango mkubwa wa punda. Punda wasingekuwepo, miji hii pia haingekuwepo,” akasema Bw Kidege.

Mohamed Shibu anasema mzigo uwe ni mzito kiasi gani ilmradi umefungwa au kutundikwa vyema kwenye mgongo wa punda wa Lamu, uhakika upo kwamba mzigo huo utafika mahali utakikanapo, haijalishi iwe ni umbali wa kiasi gani.

“Punda wetu wenyewe wamezoea kazi za sulubu. Jukumu la mwenye punda ni kuhakikisha mzigo umefungwa vyema mgongoni mwa punda. Hakikisho lipo kwamba utafika utakikanapo,” akasema Bw Shibu.

Abdalla Khalid, mmiliki na mtumiaji wa punda mwenye tajiriba ya miaka mingi anataja siri zinazowezesha punda wa Lamu kubeba mizigo mizito, ikiwemo kuhakikisha punda huyo amepewa chakula cha kutosha, afya yake kuangaliwa vyema, kumpa mnyama muda wa kutosha wa kupumzika baada ya kazi, kuepuka kumtesa kwa kumpiga mnyama akiwa kazini na pia kuhakikisha mazingira yake ya kuishi, ikiwemo boma lake ni safi.

“Kumwezesha punda wa Lamu kukuhudumia vyema, basi lazima uwe mtu wa kuheshimu haki zake zote za kimsingi. Mpe lishe bora, mpende, mpe mazingira bora na safi ya kuishi, mpumzishe baada ya kazi za siku, mpe matibabu bora nakadhalika. Chambilecho msemo tajika ‘Mtunze Punda Akutunze,” akasema Bw Khalid.

Mwanamume akimuongoza punda aliyebeba tangi la maji. PICHA | KALUME KAZUNGU
  • Tags

You can share this post!

Mradi wa Sh110 milioni wageuka makao ya panya

Ajenti wa safari za ng’ambo ashtakiwa kwa ulaghai wa...

T L