• Nairobi
  • Last Updated April 24th, 2024 12:32 PM
Vijana wa kurandaranda mtaani watupa mwili katika lango la kaunti

Vijana wa kurandaranda mtaani watupa mwili katika lango la kaunti

NA TITUS OMINDE 

KIZAAZAA kilitokea katika lango la makao makuu ya Kaunti ya Uasin Gishu pale kundi la vijana wa kurandaranda mjini Eldoret lilipotupa mwili wa mmoja wao katika lango hilo. 

Tukio hilo lilisababisha msongamano mkubwa wa magari na watu katika barabara kuu ya Uganda, inayopitia mjini humo.

Maafisa wa polisi walilazimika kutumia gesi ya vitoa machozi kutawanya vijana hao na kuepusha makabiliano yaliyonukia.

Walidai kuwa marehemu aliuliwa na askari wa kaunti kabla ya mwili wake kutupwa katika karakana moja, nyuma ya hoteli ya Assis.

Kiongozi wa kundi la chokoraa waliorekebisha tabia na maadili maarufu kama EX Street Children Bw Juma Okumu alilaani kitendo hicho, huku akilaumu askari wa kaunti kwa madai ya kuendeleza dhuluma dhidi ya chokoraa mjini humo.

“Nalaani kitendo hiki, visa vya vijana kuuawa hapa mjini vinazidi kuongezeka ambapo washukiwa wakuu ni askari wa kaunti,” alidai Bw Okumu.

Bw Akumu alitaka tume huru ya kuchunguza utendakazi wa polisi (IPOA) kuchunguza mienendo ya askari polisi pamoja na wenzao wa kaunti.

Kisa hicho kilithibitishwa na afisa mkuu wa polisi kaunti ndogo ya Turbo, Edward Masibo.

Mwili wa marehemu ulipelekwa katika hifadhi ya maiti ya hospitali ya mafunzo na rufaa ya Moi MTRH.

“Maafisa wetu walichukua mwili huo na kuupeleka katika hifadhi ya maiti ya MTRH huku uchunguzi ukianzishwa,” alisema Bw Masibo.

Visa kama hivi vimekuwa vikiripotiwa mjini Eldoret ambapo mashirika ya kutetea haki za kibinadamu yanaelekezea polisi na askari wa kaunti lawama.

Mapema mwaka huu kulitokea kisa kama hicho.

Kimutai Kirui kutoka kituo cha kupinga dhuluma dhidi ya binadamu alitaka wadau wote kushirikiana ili kzuima dhuluma za aina hiyo.

  • Tags

You can share this post!

Gachagua adai Uhuru Kenyatta alifumbia macho pombe haramu...

Gachagua: Ni heri nipoteze umaarufu kuliko kuruhusu vijana...

T L