• Nairobi
  • Last Updated April 19th, 2024 9:55 AM
Wahubiri North Rift: Tuko tayari kupigwa msasa

Wahubiri North Rift: Tuko tayari kupigwa msasa

Na TITUS OMINDE

BAADHI ya makasisi kutoka North Rift wanaunga mkono pendekezo la serikali la kupiga msasa wachungaji wote kabla ya kuwaruhusu kuanzisha makanisa kama wahubiri.

Wakizungumza mjini Eldoret siku ya Jumatatu, makasisi hao walisema wakati umefika kwa serikali kuingilia kati kwa kuwachunguza wahubiri ili kuwaondoa watu wanaojificha na wanafiki makanisani.

Wakiongozwa na Mwenyekiti wa Ushirika wa Wahubiri Eldoret Gospel Ministers, Askofu Boniface Simani, walisema kuwa kanisa limetekwa nyara na wahuni wanaonyanyasa mamilioni ya waumini ni lazima wahubiri wachunguzwe.

Akizungumza katika makao ya watoto ya Jesus Love Ministries baada ya kukabidhi zawadi za siku ya wafanyakazi kwa watoto wa makao hayo, Askofu Simani hata hivyo alionya serikali dhidi ya kutumia mwanya huo kudunisha uhuru wa kuabudu.

“Kutokana na tabia ya watu wachache miongoni mwetu, serikali italazimika kupiga msasa wachungaji. Hata hivyo, uhakiki huo usitumike kukandamiza uhuru wetu wa kuabudu,” alisema Askofu Simani.

Askofu Simani alisema tukio la kusikitisha la Shakahola, Malindi limefichua kanisa na serikali hivyo ni lazima wadau wote wawajibike kwa kuweka hatua stahiki za kuepusha matukio kama hayo siku zijazo.

Maoni yake yaliungwa mkono na askofu wa kanisa la Eldoret Integrity Church Joshua Amwaga ambaye alisema kuwa wakati umefika kwa Kenya kuiga mfano wa nchi ya Rwanda kwa kuwachunguza wachungaji wote ili kuimarisha uadilifu miongoni mwa wahudumu wa injili.

Askofu Amwaga alisema kutokana na kukosekana kwa mfumo wa kisheria wa kuwaongoza wachungaji baadhi yao wameendelea kupunja Wakenya maskini ambao wana kiu ya lishe ya Kiroho.

Huku akirejelea pendekezo hilo kwa wahubiri wahakiki, askofu Amwaga alisema Wakenya wengi wananyanyaswa na wachungaji wasio na maadili ambao wanawatorosha Wakenya maskini kwa hila.

“Wakati umefika kwa Kenya kuiga Rwanda kwa kuwachunguza wachungaji wote. Kutokana na kile kinachotokea kwa sasa miongoni mwa wahubiri ninaunga mkono uhakiki wa wahubiri nchini,” alisema Askofu Amwaga.

Askofu Amwaga alisema ni lazima wachungaji wapate mafunzo rasmi kabla ya kuruhusiwa kuhubiri makanisani.

Alisema kuwa ulimwengu unabadilika kwa kasi na kuna haja ya kuwa na sera kuhusu mahitaji ya chini ya kitaaluma kwa wachungaji kabla ya kuruhusiwa kuhubiri.

“Napendekeza kwamba kiwango cha chini cha masomo kwa mhubiri lazima kiwe stashahada ya theolojia na wahubiri wote lazima wawe na barua ya maadili mema kabla ya kuruhusiwa kuhubiri,” alisema Askofu Amwaga.

  • Tags

You can share this post!

Watupwa jela miaka 7 kwa kunaswa na jino la kiboko

Leba Dei 2023: Askofu asuta Raila Odinga kupitia maombi

T L