• Nairobi
  • Last Updated October 2nd, 2023 10:00 AM
Wahudumu wawili wa bodaboda wafariki baada ya kugongwa na lori la trela mjini Malindi

Wahudumu wawili wa bodaboda wafariki baada ya kugongwa na lori la trela mjini Malindi

NA ALEX KALAMA 

WAHUDUMU wawili wa bodaboda wamefariki papo hapo huku mmoja akiponea kifo baada ya lori la trela kutoka Mombasa kuwagonga katika eneo la BP mjini Malindi, Kaunti ya Kilifi mnamo Alhamisi.

Kulingana na kamanda wa polisi katika kaunti ndogo ya Malindi Wilmot Mwanyalo Mwakio ni kwamba ajali hiyo imetokea wakati ambapo lori lililokuwa linaaingia mjini Malindi limepoteza mwelekeo na kugonga wahudumu wa bodaboda ambapo wawili walifariki papo hapo.

Amesema dereva wa lori hilo alikuwa akijaribu kukwepa mtu aliyekuwa akivuka barabara kuu ya Malindi-Mombasa katika eneo la BP. Kwamba alishika breki ghafla asimgonge mtu huyo lakini akapoteza mwelekeo.

“Ajali hiyo imetokea mwendo wa saa kumi na moja na nusu alfajiri ambapo lori lililokuwa linatoka upande wa Mombasa limepoteza mwelekeo likagonga matatu na kuisukuma kando upande wa kushoto kisha likasonga mbele na kugonga pikipiki za bodaboda zilizokuwa zimeegeshwa kandokando ya barabara hiyo na kuwaua watu wawili papo hapo,” amesema Bw Mwakio.

Afisa huyo wa polisi ameongeza kuwa lori hilo limesonga mbele na kugonga jingine kwa nyuma. Lori lililogongwa lilikuwa limeegeshwa ili kushukisha vifaa vya ujenzi vipelekwe dukani.

“Dereva wa lori lililofanya ajali ametoroka hatujafanikiwa kumkamata lakini gari hilo limepelekwa katika kituo cha polisi cha Malindi. Pia zile pikipiki za wale waliogongwa na lori hilo zimechukuliwa na kupelekwa katika kituo cha polisi cha Malindi,” amesema Bw Mwakio.

Aidha afisa huyo wa alidokeza kuwa miili ya wawili hao imechukuliwa na kupelekwa katika chumba cha kuhifadhi maiti cha hospitali kuu ya kaunti ndogo ya Malindi ikisubiri kufanyiwa uchunguzi wa maiti.

Manusura amekimbizwa katika hospitali ya Malindi ili kupata matibabu. Amevunjika miguu na mikono.

Afisa ameeleza kwamba tayari polisi wameanzisha msako kuhakikisha wanamtia mbaroni dereva wa lori hilo ambaye yuko mafichoni.

  • Tags

You can share this post!

Rais Museveni athibitisha kuugua corona

Rais Museveni: Ambukizo la corona limesababisha likizo ya...

T L