• Nairobi
  • Last Updated November 28th, 2023 7:53 PM
Wahuni waliokuwa wakikeketa wasichana Pokot Magharibi waomba msamaha 

Wahuni waliokuwa wakikeketa wasichana Pokot Magharibi waomba msamaha 

NA OSCAR KAKAI

VITA dhidi ya ukeketaji katika Kaunti ya Pokot Magharibi vimeanza kuzaa matunda baada ya wahusika 15 kujitokeza hadharani na kutubu madhila ambayo wamekuwa wakipitishia wasichana wadogo.

Ngariba hao wa kike ambao wamekiri kubadilika, sasa wanaomba msamaha.

Kulingana nao, unyama ambao wamekuwa wakifanyia watoto wa wetu wanadai umesababisha wao kusalia nyuma kimaendeleo na hata kukosa kusoma.

Walitupa visu miezi michache iliyopita, na wanasema watakuwa balozi dhidi ya tohara kwa wanawake.

Wametoka vijiji ambavyo visa vya ukeketaji vimekita mizizi, ambavyo ni Sook, Nyarkulian, Mortome, Kamelei, Kasei, Lopetn a Cheptuya katika Kaunti ya Pokot Magharibi.

Wengine wametoka kijiji cha Kolowa, Tiaty, Kaunti ya Baringo.

Wakeketaji hao waasi wakiongozwa na Mezania Chepurai Lokudo kutoka Tamugh, Sook, ambao walikuwa wakipasha tohara wasichana wengi kwa siku moja, walisema kuwa wameamua kuacha shughuli hiyo baada ya kuemilishwa kuhusu athari zake na shirika la kijamii la Pokot Outreach Ministries (POM).

Bi Chupurai alitoa wito kwa serikali kuwasadia kupata mbinu mbadala za kujikimu kimaisha.

Alisema kuwa sasa wameona mwangaza na kugundua kuwa yale walikuwa wakifanya yalikuwa mambo mabaya.

“Tulikuwa tukiwatahiri wasichana tukifikiria kuwa tunafanya jambo nzuri, lakini tumewacha. Tumeacha shughuli hiyo haramu,” alisema.

Alisema kuwa wanao walikosa kusoma kwa sababu ya maovu hayo ambayo yalipitwa na wakati.

 “Mikono yetu nilifanya dhambi na kuathiri wasichana wetu. Wasichana hao walifanya makosa na uwezo wao kimasomo ukadidimia. Tulifikiria kuwa tunafanya wawe werevu, kumbe tunawaharibu,” alisema Bi Chepurai.

Alisema kuwa kwa sasa wamekumbatia Ukiristo na kwamba wameanza mchakato kuhamasisha wakazi dhidi ya maovu hayo katika Kaunti za Pokot Magharibi, Baringo na Uganda.

“Wakeketaji wengine wako kwa njia wanakuja kujiunga na sisi kwenye vita hii. Kanisa langu la Mafuta Pole limetufanya kuanza kusema la kwa kisu cha ngariba,” alisema.

Zipporah Kasoket kutoka eneo la Kolowa katika Kaunti ya Baringo, alisema kuwa waliamua kuasi kazi hiyo baada ya kukumbwa na changamoto nyingi.

“Ukeketaji umeharibu wasichana wetu na hawako shuleni. Wengi wanawacha masomo na kuozwa ili wazazi wapate mahari. Wazee wamekuwa wakisisitiza kupata mahari,” alisema.

Bi Kasoket alisema kuwa wasichana wengi ambao hupitia ukeketaji, huanza kunywa pombe kiholela baada ya kufurushwa na waume zao wanaposhindwa kuwalisha.

Alisema kuwa wasichana wengi wamekuwa washerati baada ya ndoa zao kufeli.

“Tunataka kuona wasichana wetu wakiwa na kazi kubwa kwenye maofisi makubwa,” alisema.

Mratibu wa Shirika la kijamii la Pokot Outreach Ministries (POM), Reuben Meriakol alisema kuwa limekuwa likisaidia akina mama walioasi ukeketaji kwa kuwapa mbuzi wabili wa kike kila mmoja, kama njia mbadala kujikimu maishani.

Bw Meriakol alilalamikia kuhusu baadhi ya machifu kuchukua mlungula na kuacha ukeketaji kuendelea.

Alidai, baadhi huchukua hadi hongo ya Sh10, 000 ili kuruhusu ukeketaji kuendelezwa.

“Tumepokea ripoti kuwa baadhi ya machifu huchukua hongo na kuruhusu ukeketaji kufanyika,” akalalamika.

Alitoa wito kwa viongozi na washikadau kuunga mkono juhudi kukomesha ukeketaji, na zaidi ya yote kushirikiana katika vita dhidi ya upashaji wanawake tohara.

“Viongozi wetu hawajafanya lolote kuhusu suala hili. Hakuna haki kwa wasichana na ukeketaji bado unaendelea. Tunataka ushirikiano,” alisema.

Afisa huyo alisema kuwa waliokuwa wezi wa mifugo wanastahili kuinuliwa na kupewa mbinu mbadala za kujikimu.

Bw Meriakol alihimiza wazazi kutoka maeneo yaliyoathirika, kuacha mila potovu kama vile ukeketaji, akilalamikia maovu hayo kuchangia ndoa za mapema.

Alisema baadhi ya waliokuwa wakeketaji sasa wamejiunga na makanisa mbalimbali.

“Mbuzi tunaowap, watawasaidia kujiendeleza kimaisha,” alisema.

Afisa huyo hata hivyo alikiri oparesheni inayoendelezwa dhidi ya ukeketaji, kupiga hatua mbele.

Kulingana na ripoti ya afya ya mwaka wa 2022, visa vya ukeketaji vimepungua kutoka asilimia38 mwaka wa 1998 hadi 15 mwaka wa 2022, na kutoka asilimia 21 mwaka wa 2014.

Kaunti ya Pokot Magharibi ina asilimia 74.

[email protected]

  • Tags

You can share this post!

Asimulia alivyonusurika kifo kwenye ajali mbaya ya barabara...

Askari wanavyohamasishwa Migori kupunguza visa vya...

T L