• Nairobi
  • Last Updated February 22nd, 2024 2:11 PM
Wakazi Tana River walalamikia kaunti kutafuna pesa za umma

Wakazi Tana River walalamikia kaunti kutafuna pesa za umma

NA STEPHEN ODUOR

WAKAZI wa Kaunti ya Tana River wameitaka serikali ya gatuzi hilo kufafanua jinsi zaidi ya Sh500 milioni zilitumika kugharamia safari za ndani kwa ndani.

Wakazi hao ambao waliandamana na mabango mjini Hola waliitaka serikali ya kaunti kuwajibikia Sh534 milioni zilizotumiwa kwa safari za humu nchini, huku vibarua wakikosa kulipwa mji huo ukikabiliwa na uhaba wa maji kwa miezi minne.

Waliishinikiza serikali ya kaunti kueleza jinsi mishahara na marupurupu ya vibarua wa kaunti hucheleweshwa kwa miezi sita, ilhali wafanyakazi wa kaunti katika ngazi za juu wanajipa starehe kwa kusafiri kila mahali bila msingi muhimu.

“Ni jambo la kushangaza kuwa ingawa hatuna maji na mishahara haijalipwa kwa miezi sita, serikali ya kaunti inatumia zaidi ya nusu bilioni kutangatanga,” alisema Zena Zuberi.

Kulingana na wakazi hao, gavana na maafisa wake wamepuuza masaibu na mapungufu yao na badala yake, wanafuja pesa katika mizunguko isiyo na faida kwenye kaunti.

Waliwakashifu viongozi kwa kile walichokitaja kuwa kutozingatia hali ya umaskini katika kaunti hiyo, kwa kusimamia vibaya rasilimali itokanayo na mgao wa fedha kutoka kwa serikali ya kitaifa.

“Pesa tunazopata kama mgao wetu sawa zisitumike kwa njia hii, matatizo yetu kama kaunti hayataki starehe bali matumizi sahihi ya rasilimali,” alisema Beatrice Njeru, mkazi.

Bi Njeru anaendelea kubainisha kuwa usafiri usio wa lazima wa viongozi wa kaunti umelazimu utoaji wa huduma duni katika kaunti, na hapana faida yoyote ya kuashiria umuhimu wa safari hizo.

Walitoa wito kwa bunge la kaunti, seneti, na bunge la kitaifa kuchukua hatua kuhusu suala hilo ili kuhakikisha kuwa kaunti inatoa hesabu kamili ya pesa hizo kwa njia inayoridhisha.

Katibu Mkuu wa Asasi ya Kiraia ya Tana River, James Rashid aliwataka viongozi hao kusikia kilio cha wakaazi hao na kutatua kero wanazozipata ama kujiuzulu.

“Tuliwaajiri maofisini na hatutakiwi kuomba huduma, hatutaomba huduma, tutakurudisha nyumbani, tutakufuta kazi kwa kuwa tuna uwezo”, alisema.

Maoni yake yaliungwa mkono na mwenzake Frankheart Daiddo, ambaye alikariri hitaji la kuwashinikiza viongozi kuwajibikia matumizi mabaya ya rasilimali za kaunti hiyo.

“Ni habari za kusikitisha, ni kiasi ambacho kingetumika vizuri katika miradi mikubwa ya maji, vituo vya afya, na ajira kwa vijana,” alisema.

Wakaazi hao waliwasilisha ombi kwa bunge la kaunti wakitaka ukaguzi wa kiasi kilichotumika katika safari hizo na kutafuta suluhu la masaibu yao ya kupata maji, mishahara na huduma zinazofaa za afya.

Pia wamemtaka mratibu mkuu wa serekali kutoipatia serekali ya kaunti ya Tana River pesa za mgao, hadi pale watakapowajibikia nusu bilioni za usafiri kikamilifu.

Kaunti ya Tana River iliorodheshwa ya nne kati ya kaunti zenye ubadhirifu katika ripoti ya mkaguzi mkuu wa hesabu za serikali iliyetolewa hivi majuzi, kwa kutumia Sh534 milioni kwa safari za ndani.

Hii ikiwa ni karibia asilimia kumi na tano ya mgao wa pesa za maendeleo katika kaunti hiyo.

 

  • Tags

You can share this post!

Fahamu chimbuko la Kiunga, mji wa Lamu Mashariki wenye...

Shabiki wa Man United kwenye mizani baada ya kuahidi kumpa...

T L