• Nairobi
  • Last Updated June 12th, 2024 4:24 PM
Wakazi waachwa gizani kwa saa 4 Al-Shabaab wakiharibu mnara wa stima

Wakazi waachwa gizani kwa saa 4 Al-Shabaab wakiharibu mnara wa stima

NA KALUME KAZUNGU

WAKAZI wa Lamu Jumatano waliachwa gizani kwa takriban saa nane baada ya magaidi wa Al-Shabaab kuuharibu mmoja wa minara ya umeme kwa kuushambulia kwa bomu.

Mnara huo wa umeme (pylon) unapatikana kati ya Milihoi na Kibokoni, Lamu Magharibi na uliharibiwa majira ya saa moja asubuhi.

Waliozungumza wanaoishi karibu na mnara huo waliohojiwa na Taifa Leo walikiri kusikia mlipuko na kisha kilichofuata baadaye ni stima kupotea.

“Tulisikia mpasuko kama wa risasi upande wa Kibokoni na Milihoi. Muda mfupi baadaye, umeme ulitoweka. Tulifahamishwa baadaye kwamba Al-Shabaab walikuwa wameharibu mmoja wa mnara wa stima maeneo hayo ambako mlipuko ulisikika,” akasema Samuel Mweni,” mkazi wa kijiji cha SabaSaba, tarafa ya Hindi, Lamu.

Maafisa wa usalama waliozungumza na Taifa Leo wakiwa kwenye eneo la tukio walisema ni kweli magaidi wanaoshukiwa kuwa Al-Shabaab waliurushia mnara kilipuzi, hivyo kuharibu vifaa muhimu vilivyopelekea stima kutoweka kote Lamu.

“Magaidi pia walijaribu kuvamia kambi ya walinda usalama Milihoi lakini wakashindwa nguvu na kutokomea msitu wa Boni. Tuko hapa kulinda mnara tukisubiri maafisa wa kampuni ya Kenya Power kufika kutathmini uharibifu uliotekelezwa na magaidi na kuangalia kama watafaulu kurudisha umeme,” akasema mmoja wa maafisa wa usalama aliyedinda kutaja jina.

Afisa mmoja wa Kenya Power aliyezungumza na Taifa Leo na kuomba kutotajwa jina alithibitisha tukio la Al-Shabaab kuvamia mnara wao wa stima na kuuharibu kwa kilipuzi, hivyo kusababisha hitilafu ya umeme kote Lamu.

Afisa huyo aidha aliahidi kufanya juu chini kuona kwamba umeme unarudishwa Lamu haraka iwezekanavyo.

“Tumeenda mbio na tayari tumefaulu kurudisha umeme wa muda Lamu baada ya masaa manne. Mnara walioharibu ni ghali na itachukua muda kuukarabati. Tunajitahidi,” akasema afisa huyo kwa njia ya simu.

Picha ya shambulio katika eneo la Widho-Mashambani mnamo Septemba 20, 2023. Stima ilipotea kwa saa nne baada ya Al-Shabaab kuharibu mnara muhimu. PICHA | KALUME KAZUNGU

Jumatano alfajiri, magaidi wa Al-Shabaab walivamia kijiji cha Widho-Mashambani, Lamu Magharibi ambako walimchinja mwanamume wa umri wa miaka 49 na kuchoma nyumba tano.

George Sumit Gitocho,  ambaye ni baba wa watoto sita, aliuawa kwa kuchinjwa na magaidi hao zaidi ya 30 waliovamia maboma ya wakazi kijijini Widho-Mashambani majira ya saa nane alfajiri ya Jumatano.

  • Tags

You can share this post!

Dorcas Gachagua: Ufukara katika familia nusra usababishe...

HII IMEENDA: Mtimkaji Mary Moraa atoka sokoni

T L