• Nairobi
  • Last Updated March 29th, 2024 8:50 AM
Wanaharakati wa mazingira wapigwa jeki mradi wa Sh20 milioni ukizinduliwa Lamu

Wanaharakati wa mazingira wapigwa jeki mradi wa Sh20 milioni ukizinduliwa Lamu

NA KALUME KAZUNGU

VIJANA wanaharakati wa uhifadhi wa mazingira katika Kaunti ya Lamu wana matumaini kwamba shughuli zao za kuhifadhi mazingira na kupigana na mabadiliko ya tabianchi zitafaulu kufuatia kuzinduliwa kwa mradi wa Sh20 milioni kupiga jeki shughuli hizo.

Mradi huo kwa jina ‘Climate Justice for Human Security’ unatekelezwa na Shirika la utetezi wa haki za binadamu la Haki Africa kwa ushirikiano na ForumCiv kutoka nchini Uswidi.

Mradi huo unalenga kusaidia jamii, hasa makundi ya vijana yanayoendeleza harakati mbalimbali za kutunza mazingira.

Unatekelezwa Lamu kwa muda wa miaka mwili.

Wakizungumza katika ukumbi wa hoteli ya Mwana Arafa mjini Lamu wakati wa uzinduzi wa mradi huo, vijana hao waliahidi kushirikiana na wadau kufaulisha mipango ya mazingira, ikiwemo kupanda miti kwa wingi na kueneza hamasa kwa jamii kujiepusha na uharibifu wa misitu.

Mwenyekiti wa Kundi la Mazingira la Lamu Environmental Forum, Mohamed Salim alitaja uzinduzi wa mradi wa Sh20 milioni kujiri kwa wakati ufaao.

Bw Salim anasema maeneo mengi ya Lamu ambayo awali yalikuwa yamesheheni mikoko yameharibiwa baada ya mamia ya miti hiyo kukatwa.

Alitaja ujenzi wa Bandari ya Lamu (Lapsset) eneo la Kililana kuwa mojawapo ya miradi iliyochangiwa mikoko kuharibiwa Lamu.

“Leo hii Lamu inashuhudia joto jingi kinyume na awali kwa sababu mazingira yameharibiwa. Mikoko mingi ilikatwa Kililana kupisha ujenzi wa Bandari. Tumekuwa tukiendeleza harakati za kutunza mazingira kwa kujitolea lakini hiyo haitoshi. Twashukuru Haki Africa kuzindua mradi unaotulenga sisi vijana. Utasaidia pakubwa kupiga jeki na kufaulisha mikakati yetu,” akasema Bw Salim.

Msemaji wa kundi la Amu Youth Conservation and Transformation Change, Abdallah Athman alisema licha ya jamii kujitahidi kuhifadhi mazingira, hasa mikoko, ipo haja ya wadau kujitokeza kuisaidia Lamu izidi kuwa na mazinfgira safi.

Washiriki wakifuatilia mawasilisho wakati wa uzinduzi wa mradi wa Sh20 milioni wa kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi na usalama. Vijana wanaolengwa kunufaika na mradi huo wameelezea matumaini yao. PICHA | KALUME KAZUNGU

Karibu asilimia 65 ya msitu wa mikoko nchini hupatikana Lamu kwa mujibu wa ripoti ya Shirika la Huduma za Misitu ncini (KFS).

“Twatarajia mradi wa Sh20 milioni uliozinduliwa leo utafaulisha azma yetu ya kutunza mazingira,” akasema Bw Athman.

Afisa Mtendaji wa Haki Africa, Hussein Khalid aliishukuru serikali ya Kaunti ya Lamu na jamii kwa ujumla kwa kukubali kufanya kazi na shirika hilo katika kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi kupitia uhifadhi wa mazingira.

“Tunaamini juhudi zaidi zitafanywa kupanda miti, hasa mikoko na mingineyo kufaulisha vita dhidi ya mabadiliko ya tabianchi na kuafikia mazingira safi kwa vizazi vijavyo,” akasema Bw Khalid.

Afisa Mkuu Mtendaji wa Haki Africa, Hussein Khalid wakati wa uzinduzi wa mradi wa Sh20 milioni wa kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi na usalama. Vijana wanaolengwa kunufaika na mradi huo wameelezea matumaini yao. PICHA | KALUME KAZUNGU
  • Tags

You can share this post!

Mwanamke mashakani kwa kuficha ‘dume’ mbakaji

Mahabusu aliyegeuza seli kuwa uwanja wa ndondi aona moto

T L