• Nairobi
  • Last Updated November 28th, 2023 7:53 PM
Warembo wa Kiislamu Lamu wataja sababu za kudinda kuolewa

Warembo wa Kiislamu Lamu wataja sababu za kudinda kuolewa

NA KALUME KAZUNGU

AKINA dada wengi wa Kiislamu wa kisiwa cha Lamu siku za hivi karibuni wamekuwa wakikwepa kuingia kwa ndoa licha ya kufikisha umri unaokubalika kisheria.

Utampata mwanadada ambaye licha ya kufikisha umri wa utu uzima, kisomo kumwezesha kupata kazi nzuri, anadinda kabisa kuingia kwa ndoa kinyume na miaka ya awali ambapo punde mwanadada alifikisha umri, alikuwa akiingia kwa ndoa mara moja baada ya kutokea mwanamume wa kumposa.

Lakini je, ni kwa nini akina dada wa miaka ya sasa kisiwani Lamu na viungani mwake kuepuka kabisa hili suala la kuolewa?

Katika kikao kilichowakutanisha wanawake Waislamu na viongozi wa dini ya Kiislamu, wakiwemo masheikh na maimamu kisiwani Lamu, ilibainika kuwa hatua ya mabinti wa sasa kujitenga na ndoa inatokana na kile kilichodaiwa kuwa ni hofu.

Bi Fatma Athman alieleza masikitiko yake kutokana na jinsi ndoa nyingi na ambazo ziligharimu fedha nyingi kufungwa zinavyosambaratika kiholela katika eneo hilo.

“Mimi mwenyewe sijaolewa na sina wasiwasi wowote. Sipangi kuingia kwenye ndoa si leo wala kesho. Yote yanatokana na madhila tunayoshuhudia kila uchao kwa wanandoa. Unapata watu wakitumia mamilioni kufunga nikahi lakini miezi michache baadaye wanakorofishana na kutalikiana. Hilo limenitia hofu mimi binafsi. Kuolewa hakunipigi mshipa tena,” akasema Bi Athman.

Bi Maryam Ali, mkazi wa Langoni kisiwani Lamu, alifananisha ndoa za kizazi cha sasa na ngoma ya watoto ambayo haikeshi.

Kulingana na Bi Ali, ipo haja ya viongozi wa dini na jamii kwa ujumla kuanzisha mafunzo maalum kwa wale wanaotaka kuoa au kuolewa ili kuwasaidia kuheshimu ndoa punde wanapooana.

Bi Ali pia hajaolewa na alisema hofu yake kuu ni kwamba huenda akaingia kwa ndoa ya majuto ikitokea kwamba mwanamume atamvunja moyo.

“Watu hawaheshimu tena hii asasi ya ndoa. Tunaoana leo tunaachana kesho. Yale tuyaonayo kila siku sisi vijana wachanga yanatutoa kabisa hamu ya kuolewa. Ni vyema viongozi wa dini na jamii kuanzisha mfumo wa kuwapokeza mafunzo mabarobaro na mabanati tunaojiandaa kuolewa au kuoa siku sijazo. Lazima mtu ukiolewa ujue umuhimu wa ndoa na kuiheshimu. Kwa sasa hilo halipo. Hali ikiendelea hivi wengi wetu tutasalia upweke,” akasema Bi Ali.

Kwa upande wake, Khadija Shee alisema kinachomzuia kuolewa ni jinsi wanaume wengi wanavyoendeleza mipango ya kando na kutoaminika kwenye ulimwengu wa sasa.

Bi Shee anasema licha ya dini yao kuruhusu wanaume kuoa mabibi hadi wanne, inachukiza kwamba wanaume wengi wamekuwa wasiri kwa wake zao, hali inayochangia migogoro ya kila mara.

“Twafahamu kwamba wanaume wa kiislamu wanaruhusiwa kuoa mke zaidi ya mmoja. Lakini lazima hili lifanyike kwa njia wazi na masikilizano na mke wa kwanza. Inakuwaje wanaume hapa wanaendeleza ndoa za siri na kudharau wake wao wa kwanza? Siolewi kamwe kama hali ni hii inayoshuhudiwa na kuwa kawaida kama ibada,” akasema Bi Shee.

Juma lililopita, Kadhi Mkuu nchini Athman Abdulhalim Hussein alizuru Lamu na kukutana na viongozi wa dini na wanawake Waislamu, ambapo alifichua kuwa talaka miongoni mwa wanandoa waislamu zimepungua kwa kiasi kikubwa.

Kulingana na takwimu kutoka kwa ofisi ya Kadhi huyo Mkuu, ni asilimia 20 pekee ya talaka ambazo kwa sasa zimerekodiwa.

“Wale wanaosema talaka miongoni mwa wanandoa waislamu zimezidi wanasukumwa na dhana tu lakini ukweli wa mambo ni kuwa tuko na asilimia karibu 20 pekee ya talaka zinazorekodiwa nchini. Tunafanya juhudi, kwa ushirikiano na viongozi wa kidini ili kuzuia hata hiyo asilimia 20 ya talaka isitokee kabisa nchini,” akasema Bw Hussein.

Akizungumza wakati wa kikao hicho, Mwenyekiti wa Baraza la Maimamu na Wahubiri wa Kiislamu (CIPK), tawi la Lamu, Abubakar Shekuwe aliwapongeza wanawake wa Lamu kwa kuwa wavumilivu na kuwaelewa waume wao hata zaidi.

Alisema hali hiyo imesaidia kupunguza pakubwa migogoro kati ya wanandoa kisiwani.

Mwenyekiti wa Baraza la Maimamu na Wahubiri wa Kiislamu (CIPK) tawi la Lamu Abubakar Shekuwe. Amewataka vijana wa kike na kiume waliofikisha umri wa utu uzima kujitolea kuolewa na kuoa bila hofu. PICHA | KALUME KAZUNGU

Bw Shekuwe aidha aliwashauri mabarobaro na mabinti waliofikisha umri wa utu uzima kutotishwa na badala yake kujitahidi kuoa na kuolewa akisisitiza kuwa kuna baraka inayokuja mara baada ya waja kuoana.

Alitaja migogoro inayozuka kwa baadhi ya wanandoa kuwa jambo la kawaida na kuwataka wakazi kukoma kuifikiria ndoa katika upande mmoja pekee wa kuanguka badala ya kutambua pia kwamba kuna nyingi zinazosimama na kunawiri.

“Kuna baadhi ya wanaume utawapata eti wanaogopa kuoa wakidai hawataki presha za maisha. Wanawake nao wanadai wanataka uhuru wao kiasi kwamba kuolewa wanakuona kuwa sawa na kujitia gerezani. Hiyo ni dhana ya ibilisi. Lazima tukubali kuwa zipo ndoa nyingi zinazofana. Kuna waliooana wakiwa chini na baadaye wakapanda kitabaka. Ndoa iko na mibaraka yake. Changamoto zilizopo zisitufanye kuogopa kuoa au kuolewa,” akasema Bw Shekuwe.

  • Tags

You can share this post!

Serikali yachunguza ‘adui wa ndani’ katika mashambulizi...

Mhubiri atupwa ndani kwa kupatikana na chang’aa

T L