• Nairobi
  • Last Updated April 20th, 2024 1:51 PM
Washukiwa 120 ndani kwa uchomaji mashine za kuchuma majani chai

Washukiwa 120 ndani kwa uchomaji mashine za kuchuma majani chai

NA VITALIS KIMUTAI

POLISI katika Kaunti ya Kericho wamewakamata zaidi ya washukiwa 120 kuhusiana na maandamano, kufungwa kwa barabara na kuteketezwa kwa mashine tisa za kuchuma majani chai katika mashamba ya kampuni ya Ekaterra.

Washukiwa hao walikamatwa katika kituo cha kibiashara cha Brooke na kijiji cha Kapsaos katika eneo bunge la Ainamoi katika operesheni iliyoingia siku yake ya tatu leo Jumamosi.

Jamaa za wale waliokamatwa walidai washukiwa hao walikuwa wamezuiliwa kwenye korokoro ya polisi kwa zaidi ya saa 24 bila kufunguliwa mashtaka.

Sheria inahitaji mshukiwa yeyote aliyekamatwa awasilishwe kortini ndani ya saa 24 au apewe dhamana.

Dhamana hiyo itamruhusu mshukiwa kupiga ripoti katika kituo fulani cha polisi baadaye kesi yake ikishughulikiwa.

“Maafisa wa vyeo vya juu Ijumaa alasiri walituambia kuwa washukiwa wamekaguliwa na Idara ya Upelelezi wa Jinai (DCI) na asilimia 80 kati yao wamebainika kuwa hawana hatia. Kwa hivyo, hao wangeachiliwa huru. Kwa bahati mbaya bado wanazuiliwa,” Bi Beatrice Bett, jamaa wa mmoja wa wale walioko korokoroni, akasema.

Kauli ya Bi Bett ilikuwa sawa na za jamaa na marafiki wengi wa washukiwa wengine, ambao walifurika katika kituo cha polisi cha Kericho mnamo Jumamosi asubuhi kufuatilia hatima za wapendwa wao.

Kampuni za James Finlays Kenya na Ekaterra zilizoko kaunti za Kericho na Bomet zimelengwa katika mashambulio ya wakazi wanaopinga matumizi ya mashine kuchuma chai na hivyo kuwanyima nafasi za ajira.

  • Tags

You can share this post!

Subirini Wi-Fi ya bure yaja katika vituo 25,000 kote nchini...

Panyako ajiuzulu nafasi yake ya Naibu Mwenyekiti UDA

T L