• Nairobi
  • Last Updated April 24th, 2024 5:50 AM
Watu wawili wafariki kwenye ajali ya matatu na trekta Ndhiwa

Watu wawili wafariki kwenye ajali ya matatu na trekta Ndhiwa

NA GEORGE ODIWUOR

WATU wawili wameaga dunia baada ya matatu kugonga trekta kwenye barabara ya Rodi Kopany-Sori katika katika eneobunge la Ndhiwa, Kaunti ya Homa Bay mnamo Jumamosi asubuhi.

Akithibitisha kutokea kwa ajali hiyo, Kamanda wa Polisi Homa Bay Samson Kinne amesema ajali hiyo imetokea katika kituo cha kibiashara cha Kobodo.

Walioshuhudia ajali hiyo wamesema matatu ilikuwa imebeba abiria wanane ikielekea mjini Homa Bay saa kumi na moja na dakika ishirini (5:20 am) alfajiri ilipogonga trekta la miwa lililokuwa limesimama katikati ya barabarani baada ya kuharibika.

Miili ya waliofariki imepelekwa katika mochari ya Manyatta Kobodo huku majeruhi wakipelekwa katika Hospitali ya Mafunzo na Rufaa ya Homa Bay. Mmoja wa manusura yuko katika hali mbaya.

Afisa wa Afya wa Kaunti Bw Kennedy Omolo anayewajibika na Mawasiliano amesema mmoja wa waliofariki ni afisa wa afya anayefanya kazi na shirika la LVCT na kwamba alikuwa mwanafunzi wa kike.

“Alikuwa mwanafunzi. Alikuwa anaenda darasani gari lilipopata ajali,” amesema Bw Omolo.

Magari hayo – matatu na trekta – yamebururwa hadi katika kituo cha polisi cha Ndhiwa.

Kamanda Kinne amewataka madereva na watumiaji wengine wa barabara wawe waangalifu ili kuzuia ajali ambazo zinaweza kuepukika.

  • Tags

You can share this post!

Serikali yatenga Sh130 milioni kupiga jeki kilimo cha miraa

Mshambuliaji Rafael Leao sasa kuchezea AC Milan hadi mwaka...

T L