• Nairobi
  • Last Updated February 22nd, 2024 1:05 PM
Watunzaji makaburi ya Lang’ata wagoma

Watunzaji makaburi ya Lang’ata wagoma

NA WINNIE ONYANDO

WAHUDUMU wa Idara ya Usafi Kaunti ya Nairobi mnamo Jumatano waliandamana wakilalamika kuwa hawajapokea mishahara yao kwa muda wa miezi mitano.

Wahudumu hao walioajiriwa na serikali ya kaunti kufanya usafi katika makaburi ya Lang’ata, walisema kuwa hawajapokea malipo licha ya kwamba wamekuwa wakitekeleza majukumu yao kwa bidii.

Maafisa wa polisi katika eneo la Lang’ata walitumia vitoa machozi kuwatawanya wafanyikazi hao.

Kulingana na kamanda wa polisi wa kaunti ndogo ya Lang’ata, Monica Kimani, maafisa walichukua hatua ya kuwatawanya waandamanaji hao baada ya kuanza kuchoma magurudumu karibu na lango la kituo cha polisi cha Lang’ata.

Kamanda huyo alisema kuwa aliwaambia wafanyikazi hao kupeleka malalamishi yao kwa afisi ya Gavana wa Kaunti ya Nairobi jijini badala ya kusababisha machafuko katika eneo hilo.

Hata hivyo, wafanyakazi hao waliapa kufunga milango ya makaburi hayo hadi wapate mishahara yao, huku wakiwataka wananchi wanaotaka kuwazika wapendwa wao kurejea nyumbani au kutafuta eneo lingine.

Akihutubia wanahabari baada ya kisa hicho, Katibu wa Kaunti ya Nairobi, Patrick Analo alithibitisha kuwa wafanyikazi hao hawakulipwa.

Alisema malipo hayo yalitatizwa na bajeti ya kaunti.

“Tuna takriban wafanyakazi 77 wanaofanya kazi kwenye makaburi ambao waliajiriwa miezi sita iliyopita ili kutunza makaburi. Niwaombe radhi kwa kuwa hawajalipwa hadi leo,” Analo alisema.

  • Tags

You can share this post!

HII IMEENDA: Mtimkaji Mary Moraa atoka sokoni

Nilikejeliwa shuleni sababu ya ‘chida ya...

T L