NA RICHARD MAOSI
WAUZAJI mafuta katika kituo cha kibiashara cha Tangakona, Kaunti ya Busia wamegeukia ukulima kukidhi mahitaji ya kila siku.
Jambo ambalo limefungua mwanya kwa shughuli za kunyonya mafuta ambayo huchuuzwa mitaani kwa bei ya jioni.
Hii ni baada ya kubainika kuwa biashara ya mafuta katika kaunti ya Busia, maeneo mengi karibu na mji zinaendelea kupoteza wateja.
Andrew Kandera mkaazi wa kijiji cha Kajoro anasema aliamua kufunga biashara yake kabisa ikizingatiwa kuwa bei ya mafuta imesalia kuwa juu.
Kulingana na Kandera, alitarajia kwamba bei ya mafuta ya petroli ingeteremka ila imebakia kuwa Sh217, dizeli Sh203, na mafuta ya taa Sh203.
“Kusema kweli wanyonyaji mafuta wametuharibia biashara na hawataki kujua kuwa pia sisi tuna familia ambazo zinatutegemea,” akasema.
Aidha, Kandera anasema wafanyibiashara wengi hasa waendeshaji boda na magari ya uchukuzi wametorokea nchi jirani ya Uganda kununua mafuta kwa bei nafuu.
Hatua hiyo inachangia mazingira ya kufanyia biashara ya mafuta Busia kuwa magumu, wauzaji wakiendelea kukadiria hasara.
Kwa upande mwingine, Kandera anasema aliamua kujitosa kwenye ukulima aliposhindwa kabisa kulipa wafanyikazi wake.
Anasema kwa siku alikuwa akinunua karibu lita 800 za mafuta, lakini katika kipindi cha miezi mitatu iliyopita biashara ya mafuta imekosa wanunuzi.
Lydia Nekesa kutoka kijiji cha Adungosi pia anasema malori ya kusafirisha mafuta kutoka nchi jirani ya Uganda ni mengi kwenye mpaka wa Kenya na Uganda.
Aidha, shughuli za kunyonya mafuta zinaonekana kurejea hasa baada ya biashara ya kuuza mafuta kuteremka nchini.
Haya yanajiri baada ya shirika la kuratibu bei ya mafuta nchini EPRA kukosa kuteremsha bei ya mafuta wiki iliyopita.
Awali, Waziri wa Kawi Bw Davis Chirchir alionya kwamba huenda bei ya mafuta ikagonga Sh300 kwa sababu ya vita kati ya Israili na Palestina ambavyo vinaendelea.