• Nairobi
  • Last Updated March 28th, 2024 11:42 PM
Wazee wa Kaya wadai kumiliki shamba la Mackenzie

Wazee wa Kaya wadai kumiliki shamba la Mackenzie

Na ALEX KALAMA

KUNDI la wazee wa Kaya eneo la Magarini, Kaunti ya Kilifi limejitokeza na kudai kumiliki ardhi yenye ukubwa wa ekari 800 ya msitu wa Shakahola inayomilikiwa na mhubiri tata Paul Mackenzie.

Wakiongozwa na Tsuma Nzai, wanasema sehemu ya ardhi ambayo inadaiwa kuwa ya Mackenzie ni mali ya wazee wa Kaya wa Magarini.

Kupitia mazungumzo na wanahabari eneo la Gongoni, wazee hao wamelaani vikali mafunzo potovu ya kiimani ambayo yalikuwa yakiendeshwa na Mackenzie na kusababisha vifo vya zaidi ya watu 200 ambao ni wafuasi wake.

Ufukuzi wa miili bado unaendelea, kundi hillo likiitaka serikali iwaachie ardhi hiyo ‘waisafishe’ pindi uchunguzi utakapokamilika.

“Ardhi hiyo ni msitu wa Kaya na tunatoa wito kwa serikali ituachilie ili tuweze kuisafisha uchunguzi ukikamilika,” alisema Bw Nzai.

Mzee huyo alisema kuwa shughuli hiyo ya kutakasa itajumuisha utafiti kuhusu jina Shakahola na maana yake ili liweze kubadilishwa.

Watalaani ardhi hiyo, kisha kuitakasa kulingana na mila na itikadi za Kimijikenda.

“Jukumu letu ni kulaani, kusafisha, kubariki na kufanya utafiti kiini cha jina Shakahola.”

Bw Nzai, aidha, alionya kuwa endapo mila hawatatekeleza mila hizo na kubadilisha jina eneo hilo litaendelea kuwa jukwaa la maafa.

Kwa upande wake mzee Said Matojo kutoka Kaya Bobo, Rabai alisema kuwa kuachwa kwa shughuli za kidini za asili za Kiafrika na kukumbatia shughuli za kidini za kigeni ndiko kunakosababisha matatizo yote yanayowakumba Waafrika.

“Serikali inapaswa kufuta usajili wa shughuli zote za kidini za kigeni ili turudi kwa utamaduni wetu wa Kiafrika ambao ulihakikisha kuwa kuna usawa na haki,” alisema Bw Matojo.

Wakati huohuo, mbunge wa Malindi Amina Mnyazi naye ameitaka serikali kuwianisha maeneo ya utawala ili kuendana na maeneo bunge akisema kuwa eneo la uhalifu la Shakahola liko katika kaunti ndogo ya Malindi kiutawala lakini kisiasa liko katika eneo bunge la Magarini.

Bi Mnyazi alipendekeza kuwa mipaka hiyo inapaswa kuangaliwa upya ili Kaunti Ndogo ya Malindi iwe eneo bunge la Malindi na Kaunti Ndogo ya Magarini iwe eneo bunge la Magarini.

Aidha mbunge huyo wa Malindi alisema kuwa inasikitisha kuona watu walikuwa wanahusisha Shakahola na eneobunge lake, ipo katika eneobunge la Magarini.

 

 

  • Tags

You can share this post!

Thailand yahalalisha bhangi licha ya sheria kali za...

Katibu Esther Ngero ajiuzulu kazi serikalini

T L